Home Sports SIMBA WAAMBULIA POINTI MOJA DAKIKA 180

SIMBA WAAMBULIA POINTI MOJA DAKIKA 180

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba kwa sasa wanapita katika kipindi kigumu kutokana na kuwa kwenye mwendo wa kuchechemea katika vita ya kusaka pointi tatu.

Ndani ya Januari kwenye mechi za ugenini wamekwama kusepa na ushindi zaidi ya kuambulia sare moja na kichapo kimoja.

Mechi mbili ambazo ni dakika 180 walikuwa kwenye msako wa pointi sita wameambulia pointi moja na kupoteza pointi tano.

Ilikuwa mbele ya Mbeya City, Uwanja wa Sokoine ambapo kipa namba moja Aishi Manula aliokota nyavuni bao moja lililofungwa na Paul Nonga dakika ya 19 likadumu mpaka mwisho wa mchezo.

Waliposepa hapo wakaibuka ndani ya Manungu, Morogoro hapo ulipigwa mpira mkubwa na mwisho wa siku wakagawana pointi moja moja kwa sare ya bila kufungana.

Katika Uwanja wa Manungu ambao ulikuwa umelowa kutokana na mvua kunyesha timu zote zilikuwa katika kasi ya kuusaka pointi tatu ngoma ikawa nzito.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanya licha ya kukosa matokeo kwenye mechi zao.

“Hatujapenda matokeo ya namna hii lakini hamna namna zaidi ni benchi la ufundi kuweza kufanyia kazi makosa kwa ajili ya kupata matokeo mazuri,”.

Kituo kinachofuata ni Kagera Sugar ni Januari 26, Uwanja wa Kaitaba.

Previous articleYANGA WAREJEA DAR NA POINTI ZA KUTOSHA
Next articleNIGERIA YATOLEWA AFCON