BEKI wa kulia wa Yanga, Djuma Shabani, amefunguka moja ya malengo yake ni kuhakikisha anatoa pasi nyingi za mabao kuanzia 15 msimu huu ambazo zitawasaidia washambuliaji wa timu hiyo kufunga mabao mengi zaidi.
Msimu huu ukiwa ni wa kwanza kwa beki huyo, tayari amefanikiwa kutoa asisti tatu ambapo mbili ni katika Kombe la Shirikisho la Azam, huku moja ndani ya Ligi Kuu Bara na kufunga bao moja.
Djuma amesema: “Ni furaha kutoa pasi ya kwanza ya bao katika mchezo wa ligi kuu, natamani kuona nikifanya hivyo kwa kutoa pasi nyingi kwenda kwa washambuliaji.
“Pasi kuanzia 15 na kuendelea ndiyo lengo langu, naona zitasaidia washambuliaji kufunga mabao, ukiongeza na pasi za wachezaji wengine basi utaona idadi nyingi ya mabao ambayo tutafunga.
“Msimu ni mgumu kwa kuwa kila timu ina malengo yake, kwetu ubingwa ndio malengo yetu ndio maana utaona kila mchezo kwetu ni mgumu kwa kuwa wapinzani wanafahamu juu ya nia yetu, lakini tunaendelea kupambana kwa ajili ya kufikia malengo,” .
Pasi yake hiyo alitoa kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji na bao lilifungwa na Fiston Mayele wakati Yanga ikishinda mabao 4-0 Uwanja wa Mkapa.