MWIJAKU AHADI YAKE MPAKA MWANASHERIA

MHAMASISHAJI wa Klabu ya Simba ambaye pia ni mtangazaji Mwijaku ameweka wazi kuwa hawezi kuzungumza ishu yoyote ile kuhusu ahadi yake ya kuweza kutembea bila nguo ambayo aliweza kuiweka hivi karibuni.

Shabiki huyo wa Simba aliweka ahadi kwamba ikiwa Klabu ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes itafungwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika angeweza kutembea bila ya nguo mpaka Sinza Mori.

Jana mambo yalikuwa ni magumu kwa Simba ambapo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 1-3 Jwaneng Galax na kufanya safari ya Simba kuishia hapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku wapinzani wao wakitinga hatua ya makundi.

Ni habari mbaya kwa mashabiki wa Simba kwa kuwa walikuwa na matarajio ya kusepa na ushindi kwa kuwa mchezo wa kwanza ugenini walishinda mabao 2-0.

Mwijaku amesema kuwa hawezi kuzungumzia jambo lolote lile kwa sasa mpaka mwanasheria wake atakapoweza kumpa ruhusa.

“Niko oves kwa sasa, nasemaje kwa sasa hivi siwezi kuzungumza jambo lolote mpaka mwanasheria wangu atakaponishauri, siwezi kuzungumza lolote mpaka mwanasheria azungumze,”.

Ilikuwa ni jana Oktoba 24, Uwanja wa Mkapa mambo yalikuwa hivyo na kuifanya Simba kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia Kombe la Shirikisho.