USITUPE NGUVU ZAKO BURE KUONYESHA TFF YA KARIA HAIJALETA AFCON TANZANIA

NIMEONA zinafanyika juhudi kubwa kuhakikisha inaonekana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hawahusiki   na lolote kwa Tanzania kupata wenyeji wa mashindano ya Afcon mwaka 2027.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limeipa Tanzania nafasi ya kuandaa Afcon mwaka 2027 pamoja na nchi mbili jirani yetu za Kenya na Uganda.

Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi hizi za Afrika Mashariki kupata nafasi hiyo ya kuandaa Afcon, jambo ambalo limekuwa ni kama matarajio ya Watanzania wengi sana.

Mwaka 2027 si mbali sana na kwa muda uliopo unatupa nafasi nzuri ya kupata maandalizi ya kutosha. Sasa ni wakati mzuri wa kuanza kupongezana na kukumbushana.

Nimeona baadhi ya watu ambao wao kawaida yao wamekuwa wakiongoza kuumizwa na baadhi ya mafanikio yanayotokea katika mpira wa Tanzania.

Ajabu kwangu, hata wale wageni katika mpira ambao inawezekana miaka minne iliyopita usingewasikia wanazungumza lolote kwa maana kuwa hawakuwepo kabisa na kama walikuwepo kwenye mpira, hawakujua lolote, leo wanaumizwa kwa kila linalofanywa na TFF.

Juhudi kubwa zinatumika kusambaza clip kadha wa kadha kuonekana zilikuwa ni ndoto za huyu au yule na wakati mwingine ikitaka kuonyeshwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dk Samia Suluhu ndiyo pekee imefanya na kufanikisha hilo jambo,

Tuachana na tabia za “roho kona” ambazo hazina sababu za msingi kwa kuwa, kwa mwendo wanaokwenda nao TFF kwa kipindi hiki na kuungwa mkono na Serikali ya Dk Samia na muunganiko wa mashabiki wengi wanaoelewa mpira unapokwenda utumia tu.

Nasema utaumia si kwa sababu utapigwa, la! Utaumia kwa kuwa maendeleo na mafanikio kadha wa kadha yataendelea kuja na wewe utaendelea kutumia muda mwingi kutaka kuonyesha TFF haihusiki, jambo ambalo halitakuwa na faida yoyote kwako.

Serikali inaweza vipi kuingia kuomba uandaaji wa mashindano ya Afcon bila ya kuhakikishiwa na shirikisho? Inawezaje kuanza hilo Serikali kabla ya shirikisho?

Watu wa shirikisho ndio wenye mawasiliano na Caf na Fifa, ndio wanaofanya shughuli zao za kila siku na mashirikisho hayo. Lakini wao ndio kiunganishi kwa Serikali.

Serikali haiwezi kujua lolote la mashirikisho hayo bila shirikisho lake. Kwa kuwa utendaji wa masuala ya soka yanafanywa na TFF na ndio mwakilishi wa Serikali kimataifa unapozungumzia mchezo wa soka.

Njia walianza kuipita ni TFF na sote tunajua na ili kufanikiwa kuandaa mashindano makubwa kama hayo nchini yanayohusisha idadi kubwa ya wageni wanaotoka nje ya Tanzania lakini fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi na kuendesha Afcon, lazima Serikali iingie.

Hapa sasa ndio tunampongeza Mama Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikubali na Tanzania ikathibitisha utayari wa kufanya mashindano haya.

Pamoja na ndoto na juhudi za TFF kutaka kuandaa Afcon, kama Serikali ya Dk Samia ingesema haiku tayari, basi wangekwama na kusingekuwa na uthubutu wa kuomba.

Lazima najua umenielewa, kuwa kila upande unastahili kupongezwa na kuna kila sababu ya kukubali kila upande ulivyofanya kazi yake na baada yah apo, muhimu liwe suala la kuungana.

Uongozi wa Rais wa TFF, Wallace Karia umekuwa na mafanikio makubwa sana. Bila shaka kwa yale mazoea ya TFF zilizopita, na tabia ya baadhi ya Watanzania wasiopenda maendeleo, basi bila shaka litakuja suala la kutaka kuonyesha hawajafanya jambo.

Watanzania wanaelewa, achaneni na kujichosha na hilo na msipoteze nguvu huku, unganeni na wadau wanaojielewa tuendelee kulipambania taifa letu katika maendeleo zaidi ya mchezo wa soka.

Kwa sasa Tanzania inazidi kupaa na mwanga unaonekana. Serikali ni kama mzazi anayemshikilia mmoja wa wanaye wanaofanya vizuri, huyu ni TFF. Matarajio ni kuwaona vijana wengine kwa maana ya mashirikisho ya michezo mingine nao wanaingia na kuendelea kuitangaza Tanzania.

Nguvu unazozitumia kutaka kuonyesha hawajafanya lolote, zitumie huku kuanza kujadili baada ya Afcon ijayo na ile waliyopata Morocco 2025, inafuatia zamu yetu. Kipi au yapi muhimu yafanyike kwa kuwa kwa mara ya kwanza inafanyika katika nchi tatu za Afrika Mashariki.