AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa nyota wao Aubin Kramo ana balaa akiwa kwenye uwanja wa mazoezi jambo linaloongeza nguvu kwenye kikosi hicho.
Nyota huyo aliyeibuka Simba akitokea ASEC Mimosas hajaonyesha makeke yake uwanjani kutokana na kusumbuliwa na majeraha alipopata maumivu wakati wa maandalizi ya Ngao ya Jamii, Mkwakwani, Tanga.
Ally amesema kuwa wachezaji wote wapo tayari kwa mechi zilizopo mbele yao ikiwa ni zile za ligi, African Football League, (AFL) na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kramo hakuwa kwenye mechi ambazo timu ilicheza kwa kuwa alikuwa bado hajawa fiti lakini kwa sasa taratibu anazidi kuwa imara kutokana na kile ambacho anakionyesha mazoezini ni balaa kubwa.
“Wale ambao walikuwa wanabeza uwezo wake watakutana naye uwanjani. Hakika kwenye mashindano yaliyopo mbele yetu wachezaji wapo tayari na burudani itaonekana kwa Wanasimba wote,” amesema Ally.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba inatarajia kucheza na Power Dynamo hatua ya pili Septemba 16 na AFL ni dhidi ya Al Ahly ya Misri Uwanja wa Mkapa Oktoba 20.