ALIYEWATUNGUA SIMBA KUIBUKIA IHEFU

NYOTA wa Coastal Union mwenye rekodi ya kuwatungua kwa pigo la penalti Simba msimu wa 2022/23 anatajwa kuibukia ndani ya Ihefu ya Mbeya.

Ni Yanga ambao ni mabingwa hawajafungwa kwa penalti kwa kuwa katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar Djigui Diarra wa Yanga aliokoa hatari hiyo.

Ikumbukwe kwamba Simba kwenye mabao 17 iliyofungwa ni bao moja pekee walifungwa kwa penalti ilikuwa Juni 9,2023 Uwanja wa Uhuru na mtupiaji wa bao ni Moubarack Amza.

Amza alipiga penalti hiyo iliyomshinda kipa namba tatu Ally Salim na mwisho ubao ukasoma Simba 3-1 Coastal Union.

Habari zinaeleza kuwa nyota huyo amemalizana na Ihefu inayofanya maboresho ya kikosi hicho kwa msimu wa 2023/24.

“Yule mtaalamu wa mapigo huru kila kitu kinakwenda sawa na Ihefu ikiwa mambo yatakamilika atatambulishwa hivi karibuni,” ilieleza taarifa hiyo.

Ofisa Habari wa Ihefu, Andrew Peter aliwahi kusema kuwa maboresho ya kikosi hicho kwa msimu ujao yatafanyika kwa umakini.