>

ARGENTINA YAFUFUA MATUMAINI KOMBE LA DUNIA

LIONEL Messi nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina amesema kuwa kwa sasa hawana chaguo ni lazima wapambane wenyewe kupata matokeo.

Nyota huyo kwa sasa ametupia mabao mawili kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya kufunga wakati ubao wa Uwanja wa Lusail Iconi uliposoma Argentina 2-0 Mexico.

Messi alipachika bao hilo dakika ya 64 na bao la pili lilifungwa na Enzo Fernandez dakika ya 84.

Nyota huyo amesema:”Tuna kazi kubwa ya kufanya na ni lazima kwa sasa tushirikiane wenyewe kupambana ili kushinda,”.

Ushindi huo unawapa matumaini Argentina ya kutusua kwenye hatua ya makundi ikiwa watashinda mchezo wao ujao kwa kuwa mchezo wa kwanza walipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Saudi Arabia.

Kwenye kundi C ni Poland wanaongoza wakiwa na pointi 4 huku Argentina wakiwa nafasi ya pili wanafuatiwa na Saudi Arabia wote wakiwa na pointi tatu na Mexico ni nafasi ya nne wakiwa hawajakusanya pointi.