DAR ES SALAAM: Klabu ya Simba SC imetangaza kuwa mashabiki wataruhusiwa kuingia uwanjani kushuhudia mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC 15 de Agosto, utakaochezwa Jumatano, Oktoba 21, 2026, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kupitia taarifa iliyotolewa Oktoba 20, 2026, na Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Simba imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya mazungumzo ya kina na FC 15 de Agosto, ambayo hatimaye imekubali ombi la kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uongozi wa Simba ulifanya juhudi kubwa za kufanya mazungumzo na wapinzani wao kwa kutambua umuhimu na thamani ya mashabiki katika mchezo wa soka, ili kuwapa fursa ya kushuhudia pambano hilo muhimu.
Aidha, Simba imetangaza kuwa kwa ajili ya kuwapa mashabiki wake fursa ya kufuatilia mchezo huo, pambano hilo litaonyeshwa kupitia televisheni kubwa (Big Screen) katika maeneo ya Mwembeyanga na Mbagala Zakheim.
Hata hivyo, klabu hiyo imeeleza kuwa taarifa kuhusu viingilio vya mchezo huo zitatangazwa baadaye.
Simba imemalizia taarifa yake kwa kaulimbiu ya “Simba Nguvu Moja!”, ikisisitiza mshikamano kati ya klabu na mashabiki wake kuelekea mchezo huo wa kimataifa.
