Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Nassor Idrissa, ametoa pole kwa familia ya marehemu Kocha Msaidizi wa Klabu ya Pamba Jiji, Themi Felix, aliyefariki dunia Oktoba 17, 2026, mkoani Mwanza.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania leo, Oktoba 18, 2026, Idrissa ametoa pole kwa uongozi wa timu, wachezaji, benchi la ufundi, familia ya marehemu pamoja na wadau wote wa soka walioathiriwa na msiba huo mzito.
Aidha, amewatakia wafiwa wote subira, uvumilivu na nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“T umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Themi Felix. Tunatoa pole kwa familia ya Pamba Jiji na wote walioguswa na msiba huu. Tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na tunawaombea faraja na nguvu ya kuhimili pengo hili kubwa,” amesema Idrissa.
Themi Felix alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, mkoani Mwanza, alipokuwa akipatiwa matibabu.
TPLB imemwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.