Atlanta United ya Marekani iko katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Uswisi, Breel Embolo, kutoka klabu ya Rennes ya Ufaransa.
Kwa mujibu wa The Athletic, Atlanta United imekubali ada ya uhamisho inayokadiriwa kufikia dola milioni 18 sawa na TSh bilioni 46.8, kiasi ambacho kitamfanya Embolo, mwenye umri wa miaka 29, kuwa miongoni mwa wachezaji watano wenye uhamisho wa gharama kubwa zaidi katika historia ya MLS.
Embolo alifunga mabao 10 na kutoa asisti tatu katika mechi 34 msimu uliopita akiwa na Rennes, ikiwa ni msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo ya Ligue 1.
Kabla ya kujiunga na Rennes, Embolo aliwahi kuitumikia AS Monaco, Borussia Mönchengladbach, Schalke 04 na Basel, ambako alianza safari yake ya soka la kulipwa.
Kwa upande wa timu ya taifa, Embolo ana mabao 26 katika mechi 92 alizoichezea Uswisi. Katika Kombe la Dunia la FIFA 2026, alicheza dhidi ya Argentina katika robo fainali, mchezo ambao Uswisi ilipoteza kwa mabao 3-1, huku Embolo akionyeshwa kadi nyekundu yenye utata.
Iwapo dili hilo litakamilika, Embolo atakuwa nyongeza kubwa kwa Atlanta United, ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya mwisho katika Eastern Conference yenye timu 15, ikiwa na pointi 12 baada ya michezo 18.