FIFA Yamtangaza Mwamuzi wa Fainali ya Kombe la Dunia 2026 Argentina vs Hispania Kesho

hirikisho la Soka Duniani (FIFA) limemtangaza mwamuzi kutoka Slovenia, Slavko Vinčić, kuwa ndiye atakayechezesha fainali ya Kombe la Dunia 2026 kati ya mabingwa watetezi Argentina na Hispania, itakayopigwa kesho Jumapili Julai 18, 2026.

Vinčić mwenye umri wa miaka 46 anapewa jukumu hilo miaka miwili baada ya kuchezesha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) mwaka 2024, ambapo Real Madrid iliifunga Borussia Dortmund mabao 2-0.

Katika Kombe la Dunia la mwaka huu, Vinčić amechezesha michezo mitatu, akitoa jumla ya kadi saba za njano na kadi moja nyekundu, huku akiwa hajatoa penalti hata moja.

Mchezo wake wa hivi karibuni ulikuwa hatua ya 32 Bora, ambapo alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki wa Ecuador, Piero Hincapié, baada ya mapitio ya VAR kufuatia tukio la ugomvi dhidi ya mchezaji wa Mexico. Pia alichezesha sare ya 1-1 kati ya Brazil na Morocco pamoja na ushindi wa Algeria wa mabao 2-1 dhidi ya Jordan katika hatua ya makundi.

Uteuzi wa Vinčić unakuja wakati FIFA ikikabiliwa na ukosoaji kuhusu baadhi ya maamuzi ya waamuzi yaliyodaiwa kuibeba Argentina katika michuano hiyo. Miongoni mwa matukio yaliyolalamikiwa ni Lionel Messi kuepuka kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya mchezaji wa Algeria, huku makocha wa Misri na Afrika Kusini wakidai kuwepo kwa kutokuwapo kwa usawa katika maamuzi.

Hata hivyo, Mkuu wa Waamuzi wa FIFA, Pierluigi Collina, alitetea waamuzi wa mashindano hayo akisema hakuna anayepaswa kuhoji uadilifu wao.

Katika msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Vinčić pia alichezesha robo fainali ya kusisimua kati ya Bayern Munich na Real Madrid iliyomalizika kwa Bayern kushinda mabao 4-3. Katika mchezo huo alitoa kadi tano za njano kwa wachezaji wa Madrid na kuwapa Eduardo Camavinga na Arda Güler kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi za pili za njano.

Uteuzi wa mwamuzi huyo pia umeibua mjadala kutokana na mvutano unaoendelea kati ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, na Rais wa UEFA, Aleksander Čeferin, ambaye pia anatokea Slovenia.

Vinčić anafuata nyayo za mwamuzi wa Poland, Szymon Marciniak, aliyechezesha fainali ya Kombe la Dunia 2022 kati ya Argentina na Ufaransa nchini Qatar.

Aidha, uteuzi huo unaendeleza utaratibu uliodumu kwa Kombe la Dunia 10 mfululizo tangu mwaka 1990, ambapo FIFA imekuwa ikiteua waamuzi kutoka Ulaya kuchezesha fainali zinazofanyika nje ya bara hilo, huku waamuzi kutoka mabara mengine wakipewa fainali zinazochezwa Ulaya.