Yanga SC hesabu kubwa kwenye CRDB Federation Cup

UONGOZI wa Yanga SC umebainisha kuwa dhamira kubwa iliyopo kwa sasa ni kupambana kulitetea taji la CRDB Federation Cup wakiwa wapo hatua ya nusu fainali.

Juni 21, 2026 Yanga SC itashuka Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kusaka tiketi kutinga hatua ya fainali dhidi ya Azam FC, mshindi kwenye mchezo huu atakutana na Simba SC, hatua ya fainali.

Ali Kamwe, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga SC mesema dhamira kubwa ni kutetea kombe la Shirikisho.

“Kombe la Shirikisho la CRDB kwa sasa lipo mikononi mwetu kama mabingwa watetezi. Dhamira yetu sote ni kuona Yanga inalitetea taji hili na kutwaa ubingwa kwa mara ya tano mfululizo. Hata hivyo, azma hiyo haitafikiwa kwa urahisi bila sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wetu. Ndiyo maana nawasisitiza kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho ili kuwapa nguvu na hamasa wachezaji wetu.

“Ratiba ya mashindano imekuwa ngumu na yenye msongamano mkubwa, huku kila mchezo uliobaki ukiwa na umuhimu wa kipekee. Katika kipindi hiki, wachezaji wetu wanahitaji sana sapoti yetu, na sauti zetu kutoka majukwaani zina mchango mkubwa katika kuwapa morali ya kuendelea kupambana kwa nguvu zote.

“Kesho ni siku muhimu kwa familia ya Wananchi. Amka mapema, jiandae vizuri, vaa kwa nadhifu na uje na familia yako, marafiki au mpenzi wako. Tukutane kwa wingi Uwanja wa CCM Kirumba kuisapoti na kuipambania YANGA yetu. Kwa pamoja, tuonyeshe nguvu ya Wananchi na tuwe sehemu ya safari ya kuelekea kutetea ubingwa wetu.”