Kesi inayomhusu mchezaji Mohammed Damaro Camara kuhusu uhalali wake wa kucheza kama raia wa Tanzania inasikilizwa leo na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.
Shauri hilo limefunguliwa na Simba ambao wamepinga usajili wa mchezaji huyo kwa madai kuwa umefanyika kinyume na taratibu za FIFA kuhusu ubadilishaji wa uraia wa wachezaji (Switching of Nationality).
Kwa mujibu wa Simba, kanuni za FIFA zilipaswa kufuatwa kikamilifu katika mchakato huo, wakidai kuwa mamlaka za ndani hazina kanuni maalum zinazosimamia ubadilishaji wa uraia, hivyo kuacha mwanya wa ukiukwaji wa taratibu hizo.
Taarifa zinaeleza kuwa suala hilo tayari limefikishwa pia kwa FIFA ili lifanyiwe uchunguzi zaidi na kutoa mwongozo sahihi kuhusu uhalali wa mchezaji huyo.
Kesi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia za wadau wengi wa soka nchini, huku matokeo yake yakitarajiwa kuwa na athari kubwa katika usimamizi wa masuala ya uraia na usajili wa wachezaji katika ligi za Tanzania.