Winga wa England, Jadon Sancho, alionekana jijini Paris akiwa ameshikana mikono na mpenzi wake, rapa wa Marekani Saweetie, katika tukio lililoonyesha wazi mahusiano yao hadharani.
Sancho, anayekipiga kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa akitokea Manchester United, alionekana akiwa amevalia beanie nyeusi, jaketi la ngozi, fulana nyeusi na jeans, huku Saweetie (32) akivutia kwa koti la kahawia na gauni la mosaic lenye mpasuo mdogo.
Tetesi za wawili hao kuhusiana zilianza mwaka jana baada ya Saweetie kuonekana kwenye wallpaper ya simu ya Sancho. Tangu hapo, wameonekana mara kadhaa pamoja, na Sancho aliongeza ishara zaidi kwa kuchora tattoo ya jina “Quiava” (jina halisi la Saweetie ni Diamonte Quiava Valentin Harper) nyuma ya sikio lake mwezi Agosti.
Pia alifunika tattoo yake ya zamani iliyosomeka “Her only” kwa mchoro wa maua.
Saweetie alijizolea umaarufu mkubwa tangu albamu yake ya kwanza mwaka 2017. Wimbo wake Icy Girl ulipata hadhi ya double platinum, na ametoa pia High Maintenance, huku akitarajia kuachia albamu mpya Pretty Btch Music mwaka huu.
Sancho alikuwa Paris kupumzika baada ya Villa kupoteza 3-1 dhidi ya Newcastle United katika raundi ya nne ya FA Cup. Alicheza dakika 12 pekee chini ya kocha Unai Emery.
Ingawa Villa hawana ulazima wa kumnunua mwishoni mwa mkopo wake, Emery hivi karibuni alimsifu akimuita “mchezaji wa kipekee,” na kufungua uwezekano wa kusajiliwa moja kwa moja iwapo ataonyesha kiwango chake bora.
Kwa sasa, Sancho anaonekana kufurahia maisha nje ya uwanja huku mustakabali wake kisoka ukiendelea kujadiliwa.
