Ivory Coast Watolewa AFCON 2025, Misri Watinga Nusu Fainali

Mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), Ivory Coast ‘The Elephants’, wameaga rasmi michuano hiyo baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Misri ‘Mafarao’ katika mchezo wa robo fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Adrar.

Misri walionyesha dhamira kubwa ya kutwaa taji hilo kwa mara nyingine, wakipata mabao yao kupitia Omar Marmoush (dk 3), Ramy Rabia (dk 32) na nyota wao Mohamed Salah (dk 54). Ivory Coast walijibu mashambulizi kwa mabao mawili, likiwemo bao la kujifunga la Fatouh (dk 40) pamoja na bao la Doue (dk 73), lakini juhudi hizo hazikutosha kuwazuia Mafarao kusonga mbele.

Matokeo hayo yameiwezesha Misri kufuzu hatua ya nusu fainali, ambapo sasa watakutana na Simba wa Teranga, Senegal, katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali na wenye ushindani mkubwa.

Kwa upande mwingine, kuondolewa kwa Ivory Coast kunamaanisha kuwa bingwa mtetezi hatalinda taji lake, hali inayoacha michuano ya AFCON 2025 ikiwa wazi zaidi kwa timu zilizosalia kupigania ubingwa.

RASMI: Ratiba ya Nusu Fainali AFCON 2025

Januari 14, 2026

  • 20:00 – Senegal 🇸🇳 vs 🇪🇬 Misri

  • 23:00 – Nigeria 🇳🇬 vs 🇲🇦 Morocco

Mashabiki wa soka barani Afrika wanatarajia michezo miwili ya nusu fainali itakayojawa na presha, historia na ndoto ya kulinyakua taji la AFCON 2025.