NDANI ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25 kuna timu mbili ambazo ukuta wao kwenye eneo la ulinzi ni pasua kichwa kwa benchi la ufundi kutokana na kuruhusu mabao mengi uwanjani.
Safu ya ulinzi namba moja ambayo imeruhusu mabao mengi ni Fountain Gate ambayo imetunguliwa jumla ya mabao 43 huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ikifunga mabao 28.
Fountain Gate kwenye msimamo wa ligi ni namba 8 ikiwa imekusanya jumla ya pointi 28 sawa na idadi ya mabao ambayo yamefungwa na timu hiyo.
Kwenye mchezo wake uliopita dhidi ya Singida Black Stars uliochezwa Aprili 2 2025 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Fountain Gate 0-3 Singida Black Stars, mabao matatu na pointi zilikuwa ni mali ya Singida Black Stars.
Ni mechi 24 Fountain Gate imecheza ikiwa imekomba dakika 2,160 ina wastani wakuokota mpira nyavuni kila baada ya dakika 50.
Issa Liponda, maarufu kwa jina la Mbuzi ameweka wazi kuwa makosa yaliyopita yatafanyiwa kazi ili timu hiyo kuwa imara kwenye mechi ambazo wanacheza.
“Ushindani ni mkubwa na tunatambua kwamba kila timu inahitaji ushindi, makosa yaliyopita tutafanyia kazi ili kuwa imara mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kazi inaendelea.”
Timu namba mbili kuruhusu mabao mengi ni Ken Gold ambayo ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo baada ya mechi 16 ni mabao 42 safu ya ulinzi imeruhusu huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 20.
Kwenye dakika 2,160 ambazo Ken Gold imeshuka uwanjani ina wastani wakuokota mpira nyavuni kila baada ya dakika 51.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.