UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa umefurahi kulipa kisasi dhidi ya timu ambazo zilifungwa na Tabora United kwenye mechi za ushindani ambazo zilichezwa msimu wa 2024/25 ndani ya uwanja.
Simba imecheza mechi 16 za Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC ikiwa ni ligi namba nne kwa ubora Afrika. Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni namba moja kwenye msimamo ikiwa na pointi 43 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 42.
Fabruari 2 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulisoma Tabora United 0-3 Simba kwa mabao ya Leonel Ateba ambaye alifunga mabao mawili dakika ya 12 na 33 huku bao moja likifungwa na Shomari Kapombe dakika ya 65 akitumia pasi ya Ateba.
Ateba kwenye mchezo huo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kwa kuhusika kwenye mabao yote matatu yaliyofungwa na timu hiyo.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wamelipa kisasi kwa timu zote za Dar ambazo zilifungwa na Tabora United kwenye mechi za ligi ndani ya dakika 90.
“Tumelipa kisasi kikatili mbele ya Tabora United kwa kupata pointi tatu na ushindi huu ikiwa ni furaha kwetu huku wale waliofungwa na timu hii tukiwalipia kisasi hivyo kwa sasa Dar ipo salama.
“Ni mchezo uliokuwa mgumu unaona kwamba Tabora United ina timu imara na yenye ushindani lakini tumepata matokeo hivyo kwa wale waliofungwa watakuwa wamefurahi. Kwa kilichotokea kwa sasa Tabora United tunawapa ruksa kurudia kuwafunga tena wale waliowafunga kwa kuwa kazi yetu sisi tumekamilisha.”
Ndani ya msimu wa 2024/25 Simba imevuna pointi sita mbele ya Tabora United na kufunga mabao sita huku safu ya ushambuliaji ya Tabora United ikiwa haijaifunga Simba kwenye ligi.
Timu ambazo Tabora United ilipata kuzifunga kwenye ligi ambazo zipo ndani ya tatu bora ni Azam FC na Yanga.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.