SOKA la Wanawake linazidi kukua kila iitwapo leo kutokana na wachezaji kupata fursa ya kucheza kitaifa na kimataifa. Yote haya yanatokana na jitihada ambazo zinafanyika kila siku kwenye kupunguza changamoto huku rushwa ya ngono ikitajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazodumaza vipaji hivyo ni muhimu kwa wahusika kutoipa nafasi kuokoa vipaji vingi.
Suala la ukatili kwa wachezaji wa kike nalo linapaswa kuwekwa kando ambapo moja ya viongozi wa timu wamebainisha kuwa linatokana na wale wanaotenda hayo kutokuwa na hofu ya Mungu, tamaa pamoja na kutofuata maadili ya kazi jambo ambalo linapaswa kupingwa.
Tumefanya mazungumza na viongozi wa timu mbalimbali kutambua namna ambavyo wanaishi na wachezaji kambini pamoja na kutatua kesi zinazohusu ukatili wa kijinsia namna hii:-
Issa Liponda, Ofisa Habari wa Fountain Gate amebainisha kuwa rushwa ya ngono kwenye kupatikana mikataba ya wachezaji wa kike ni chagamoto ambayo inadumaza vipaji vya wengi kwa kuwa wapo ambao huamua kuacha kucheza mpira wanapokutana na kadhia hiyo. Huyu hapa anafunguka:-
“Vipaji vingi vinapotea kutokana na suala la baadhi ya viongozi ambao sio waadilifu kuomba rushwa ya ngono ili wawape mikataba wachezaji, hili jambo linapaswa kuachwa kabisa ili kuokoa vipaji na kuendeleza maendeleo katika soka la Wanawake. Kuna visa ambavyo viliwahi kutokea na vipo, kuna mchezaji ambaye alikutana na jambo hilo kwenye moja ya timu alikubalika kutokana na kipaji chake ila ilipofika suala la kupewa mkataba mambo yakawa mengi.
MFUMO WA UTOAJI MIKATABA UPOJE?
“Ifahamike kwamba mikataba ni makubaliano ya pande zote mbili kwa hiyo mikataba ambayo wachezaji wa kike wanaingia ni sawa na ile ambayo wachezaji wakiume wanaingia hapo kunakuwa na vipengele tofauti ikiwa ni malipo ya mshahara, bonus na vipengele vingine mbalimbali?
MIKATABA YAO IMEWAHI KULETA MATATIZO?
“Katika uelewa mchezaji anaweza kuingia mkataba na timu kuwa anapaswa kulipwa kiwango fulani cha fedha baada ya muda unaweza kupita hajalipwa. Wakati mwingine mchezaji anasaini anashindwa kuripoti kambini kutokana na matatizo mbalimbali. Haya yanatokea na yanafanyiwa kazi kwa mazungumzo kama ambavyo mkataba unazungumza.
KATIKA UTOLEWAJI MIKATABA SUALA LA RUSHWA LA NGONO LIMEWAHI KUHUSISHWA KWA WACHEZAJI WA KIKE?
“Kuhusu suala la kuwarubuni wachezaji ili kuwapa mikataba ipo na kuna viongozi ambao wanafanya hivyo kwa kuwasiliana na wachezaji mpaka wazazi. Ambacho kinatokea mchezaji anaahidiwa mengi na mwisho anaombwa rushwa ya ngono hapa mchezaji msimamo wake utaamua awe kundi lipi.
“Hii tabia sio nzuri kwa kuwa inadumaza maendeleo ya soka, wapo wachezaji ambao huacha kucheza kutokana na usumbufu wa kuombwa rushwa ya ngono hivyo wenye tabia hizi wanapaswa kuacha mara moja.”
BOSI CEASIAA QUEENS FC HUYU HAPA
Cecilia Haule, Mtendaji Mkuu wa Ceasiaa Queens FC ameanza kwa kufafanua namna hii: “Kwanza ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka ambalo hadi sasa Serikali, taasisi binafsi, vyombo vya ulinzi na usalama pia mtu mmojammoja tunapambana ili kutokomeza.
“Binafsi sijawahi kuletewa au kukabiliwa direct, (moja kwa moja) na jambo hili japo nalifahamu na kimsingi napinga sana mambo hayo kwasababu hayana afya katika jamii na hasa katika Soka la Wanawake.
MNAISHI NAMNA GANI NA WACHEZAJI MKIWA KAMBINI?
“Tunaishi kwa kufuata misingi na taratibu tulizojiwekea lakini pia kwa kufuata program maalumu kwa ajili ya mchezo husika.
KUNA ELIMU AMBAYO HUWA MNATOA KWA WACHEZAJI KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA?
“Tunafanya hivyo kwa kuwa kuna wakati tunaalika dawati la jinsia kutoka makao makuu ya Polisi Iringa pia huwa tunawaarika Wanasaikolojia kutoka chuo kikuu cha Iringa ili kutoa elimu.
SABABU ZIPI ZINABABISHA UKATILI WA KIJINSIA HASA WA NGONO?
“Nadhani sababu kubwa ni tamaa na kukosa hofu ya Mungu na ndiyo maana kwetu tumeweka kanuni mbalimbali zinazopinga ukatili, ukivunja iwe ni kiongozi au mchezaji adhabu yake ni kufukuzwa mara moja, bahati nzuri haijawahi tokea.
MAZINGIRA YA KAMBI YAPOJE KIUJUMLA?
“Tumeweka katika ubora wake kwa kuhakisha vijana wanapata mahitaji yote ya msingi ya binadamu kuishi kwa maana ya chakula, maladhi pamoja haki zao nyingine.”
KOCHA WA MPIRA HUYU HAPA
Kwa upande wa kocha wa Alliance Girls ya Mwanza, Ezekiel Chobanka amebainisha kuwa wamekuwa wakizunguma na wachezaji ili kuwapa elimu kuishi kwenye maadili mazuri.
“Tunaishi nao kwa kuzingatia miiko na kazi kubwa tunayoifanya ni kuzungumza nao kwakuwa hawa ni mabinti zetu lazima tuwafundishe kuwa na maadili mema kesho watakuwa kwenye familia.
“Kuhusu kupata kesi za ukatili wa kijinsia hasa wa kingono hapana haijawahi tokea hii inatokana na mazingira ambayo tunaishi nao. Kwanza wao wapo camp, (kambini) yao sisi tupo mbali nao isipokuwa huwa tunakutana kwenye maongezi kabla ya mechi.
KWA NINI MAKOCHA WA KIUME KUTAJWA SABABU YA UKATILI WA KIJINSIA?
“Nadhani hiyo inatokana na kutokujitambua maana kama unafahamu maadili ya kazi huwezi fanya mambo hayo, hao lazima uwachukulie kama wanao.”
DENSA MSIKIE
Nyota anayecheza kikosi cha Simba Queens, Fatuma Issa, maarufu kama Fety Densa ambaye mbali na kucheza mpira ni mjasiriamali anayeuza sabuni na nguo za kisasa zenye nembo ya DENSA ameweka wazi kuwa wamekuwa wakipewa semina ambazo zinawajenga kuhusu masuala ya kijinsia huku upande wa mikataba kukiwa na vipengele tofauti.
“Kuna semina ambazo huwa zinatolewa japo sio mara kwa mara lakini huwa zinatuimarisha. Kuhusu mikataba kuna vipengele vingi ambavyo vipo.”
Makala haya yameandikwa na Lunyamadzo Mlyuka na Lulu Mpalanzi.
Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.