>

‘WALIOTUMWA NA AFANDE’ WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA

Mahakama ya Hakimu Mkazi (Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki) iliyopo mkoani Dodoma leo Septemba 30, 2024 imewahukumu kifungo cha maisha jela Washtakiwa wanne baada ya kuwakuta na hatia katika makosa yote mawili walioshtakiwa ikiwemo kosa la kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile Binti Mkazi wa Yombo Dovya, Jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 ilikuwa inawakabili Washtakiwa wanne akiwemo MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo ambaye ni Askari wa JWTZ, C.1693 Praygod Mushi aliyekuwa Askari Magereza, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Kesi hii maarufu ‘Waliotumwa na Afande’ imesikilizwa faragha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ambapo upande wa Jamhuri uliwasilisha Mashahidi 18 na vielelezo 12 kuthibitisha mashtaka dhidi ya Washtakiwa.

Washtakiwa walifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile Binti huyo ambaye Mahakamani anatambulika kwa jila la XY ambapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, baada ya kusomewa mashataka yao walikana na kutokana na unyeti wa kesi hiyo hawakupatiwa dhamana

Aidha, baada ya kesi kusikilizwa kwa siku kadhaa leo wamesomewa hukumu na kukutwa na hatia hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha.