>

TAIFA STARS KAMILI GADO KUIVAA ETHIOPIA

BENCHI la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars limeweka wazi kuwa maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Ethiopia yapo vizuri kwa kila mchezaji kuwa tayari kuipambania jezi ya Tanzania.

Ni Septemba 4 2024 Taifa Stars inatarajiwa kushuka Uwanja wa Mkapa kwa ajili ya mchezo huo wa kuwania kufuzu AFCON 2025 itakuwa ni saa 1:00 usiku.

Juma Mgunda, Kocha msaidizi wa Taifa Stars amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kwa wachezaji kuwa tayari kuelekea mchezo huo dhidi ya Ethiopia.

“Kuhusu mchezo wetu dhidi ya Ethiopia maandalizi yako vizuri ninaweza kusema kuwa kwa zaidi ya asilimia 80 yamefikia tunaendelea kujiandaa ili kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu, wachezaji wapo tayari kuona wanafanya vizuri uwanjani.”

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Cliford Ndimbo amesema kuwa kikosi kinaendelea na maandalizi vizuri huku kila kitu kikiwa kwenye mpangilio hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Septemba 4 Uwanja wa Mkapa.

“Wachezaji wana ari kubwa kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Ethiopia na mechi wanaitaka hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa kushuhudia burudani.”

Miongoni mwa wachezaji waliopo timu ya taifa ya Tanzania ni Feisal Salum, Himid, Dickson Job, Ally Salim.