>

CBE WA ETHIOPIA MABINGWA WA KOMBE LA CECAFA LA WANAWAKE

Baada ya kushindwa katika fainali mara mbili, timu ya kocha Birhanu Gizaw Heye imefanya vyema baada ya kuilaza Kenya Police Bullets 1-0 kwenye fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Abebe Bikila mjini Addis Ababa na kubeba Kombe la Cecafa kwa upande wa Wanawake.

Mfungaji bora wa shindano hilo Senaf Wakuma Zenaf Demise alifunga bao pekee dakika 79 baada ya timu yake kutawala mchezo kutoka mwanzo. Timu ya Kenya ambayo ilikuwa ikicheza fainali ya kwanza katika mchuano huo ilitumia mbinu ya kujilinda huku timu ya CBE ikizidisha shinikizo zaidi.

Mwaka 2021 CBE ilipoteza katika fainali dhidi ya Vihiga Queens ya Kenya, na mwaka jana ilipokea kichapo kingine kutoka kwa JKT Queens ya Tanzania katika fainali iliyochezwa Uganda.

Mfungaji wa goli hilo Zenaf Demise aliyemaliza akiwa na mabao sita alisema alifurahi sana kufunga mabao mengi yaliyoisaidia timu yake kutwaa Kombe. “Tuna furaha sana na tutasherehekea kombe hili kwa muda mrefu,” aliongeza mshambuliaji huyo.

Michuano hiyo ilishirikisha timu nane kutoka Ethiopia, Uganda, Tanzania, Burundi, Djibouti, Sudan Kusini, Kenya na Rwanda.