UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa kazi kubwa kwenye anga la kimataifa itakwenda kuamuliwa Dar, Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wa marudio dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.
Ni Septemba 15 2024 baada ya dakika 90 kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ubao ulisoma Al Ahli Tripoli 0-0 Simba hivyo ndani ya dakika 90 hakuna mbabe aliyepatikana kati yao uwanjani.
Meneja wa Idara ya Habari wa Simba, Ahmed Ally licha ya timu hiyo kukosa ushindi ameweka wazi kuwa matokeo hayo ni mazuri vibaya mno ugenini hivyo watafanya kazi kubwa kwenye mchezo wa marudio Uwanja wa Mkapa kupata ushindi ndani ya dakika 90.
“Haya matokeo ambayo tumeyapata ugenini ni matokeo mazuri vibaya mno na kwenye mchezo wetu tutakaocheza nao Uwanja wa Mkapa Septemba 22 matokeo yataamuliwa hapo. Wachezaji tupo tayari na tunakwenda kufanya kazi kubwa uwanjani.”
Shomari, Kapombe beki wa Simba ameweka wazi kuwa watafanya kazi kubwa kweye mchezo ujao wakiwa nyumbani katika anga la kimataifa.
“Tulicheza kwa maelekezo ya benchi la ufundi tunaamini kwamba tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu ujao nyumbani. Kucheza ugenini kuna utofauti na mbinu pia ni tofauti.”