PARIS YANGA’A WAKATI WA UFUNGUZI YA MICHEZO YA OLIMPIKI

Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2024 imefunguliwa mjini Paris kwa mbwembwe na mtindo wa kipekee huku mamia ya wanariadha washiriki wakiabiri maboti katika mto Seine katikati ya burudani la kukata na shoka la muziki.
Hafla hiyo ya ufunguzi imetoa fursa adimu ya kuuonyesha utamaduni wa Ufaransa, fasheni na muziki japo ilikumbwa na kiwingu cha mvua. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, hafla ya ufunguzi haikufanyika ndani ya uwanja kama ilivyozoelekea bali kwenye Mto Seine katikati ya mji mkuu Paris.

Wanamuziki tajika duniani Celine Dion, Lady Gaga, nyota wa muziki wa RnB Aya Nakamura miongoni mwa wengine walitumbuiza maelfu ya mashabiki waliostahamili kishindo cha mvua ili kushuhudia moja kati ya ufunguzi wa hafla kubwa za michezo duniani.
Zaidi ya wakuu 100 wa nchi walihudhuria hafla hiyo ya ufunguzi akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mke wa Rais wa Marekani Jill Biden miongoni mwa viongozi wengine.