AZIZ KI NA FEI WANA REKODI ZAO BONGO

KIUNGO mshambuliaji ndani ya Azam FC, Feisal Salum, maarufu kama Fei Toto anaingia kwenye orodha ya nyota waliofunga hat trick mapema ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24. Huku mwamba Aziz Ki wa Yanga akiingia kwenye rekodi ya nyota aliyefunga hat trick nyingi ambazo ni mbili.

Mbali na Fei  kuwa mfungaji wa hat trick ya mapema ni yeye alifungua pazia la mastaa waliofunga hat trick ndani ya ligi iliyogota mwisho Mei 28 2024 huku mabingwa wakiwa ni Yanga na walimaliza wakiwa na pointi 80.

Mabao hayo matatu kiungo huyo Fei Toto mwenye tuzo ya kiungo bora wa msimu aliyotwaa kwenye usiku wa Tuzo za Wanamichezo Zanzibar alifunga kwenye mchezo dhidi ya Tabora United ambayo ina uhakika wa kushiriki ligi msimu ujao wa 2024/25.

Alifunga mabao hayo dakika ya 3, 9 na 12 mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ambapo timu hiyo ilitwaa pointi tatu mazima.

Jumla aligotea kwenye mabao 19 akiwa namba mbili kwa wakali wa kucheka na nyavu huku namba moja akiwa ni Aziz Ki wa Yanga ambaye ana rekodi ya kuwafunga hat trick Azam FC kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Mkapa.

Hat Trick ya pili Aziz Ki aliwatungua Tanzania Prisons kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni funga kazi Mei 28 2024 alipokamilisha kwa kufunga jumla ya mabao 21 akisepa na tuzo ya mfungaji bora.