HIVI NDIVYO CHAMA ALIVYOKWAMA SIMBA

KIUNGO wa Simba, Clatous Chama amekwama mazima ndani ya Simba kuifikia rekodi yake ya kuwa namba moja katika kutengeneza pasi za mwisho ndani ya ligi kwa msimu wa 2023/24.

Ikumbukwe kwamba Chama raia wa Zambia msimu wa 2022/23 alikuwa ni namba moja kwa wakali wa pasi za mwisho alipotoa jumla ya pasi 14 na kufunga mabao manne.

Ni mechi 21 alicheza Chama akikomba dakika 1,913 hivyo alihusika kwenye mabao 18 yaliyofungwa na Simba iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya pili alikuwa na hatari kila baada ya dakika 91.

Ngoma imekuwa nzito msimu wa 2023/24 ambapo ndani ya ligi ni mabao 7 kafunga akitoa pasi 6 za mabao hivyo kahusika kwenye mabao 13 yaliyofungwa na timu hiyo.

Kakomba dakika 1,610 akicheza mechi 21 akiwa na hatari kila baada ya dakika 123 jambo linaloonyesha kuwa msimu wa 2023/24 haukuwa bora kwa mwamba Chama huku Simba ikigotea nafasi ya tatu na pointi 69.

Nyota huyo kwa sasa mkataba wake umegota mwisho ndani ya Simba ambapo inatajwa kwamba yupo kwenye mazungumzo na mabosi wa timu hiyo ili aongeze kandarasi mpya.