ZIMBWE JUNIOR: HATUJAFIKIA MALENGO

NAHODHA msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein Zimbwe Junior ameweka wazi kuwa hawajafikia malengo yao ndani ya msimu wa 2023/24 kwenye Ligi Kuu Bara.

Ipo wazi kwamba Simba imepishana na mataji yote muhimu kuanzia Ligi Kuu Bara, CRDB Federation cUP na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Itashiriki Kombe la Shirikisho msimu wa 2024/25 baada ya kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu na pointi 69 huku Azam FC na Yanga hizi zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo wa funga kazi ilikuwa ni Mei 28 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 2-0 JKT Tanzania ambapo Zimbwe alianza kikosi cha kwanza na kukomba dakika 90.

Nyota huyo chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Juma Mgunda ameweka wazi kuwa hawajafikia malengo yao kwa asilimia kubwa.

“Malengo yetu kwa asilimia kubwa hayajatimia kwa kuwa tulikuwa tunahitaji kufanya vizuri msimu wa 2023/24 ila mwisho imekuwa hivyo,tuna amini kwamba msimu ujao Mungu akipenda tukiwa wazima tutafanya vizuri.

“Mashabiki tunawashukuru kwa kuwa wamekuwa pamoja nasi mwanzo wa msimu mpaka mwisho wa msimu bado kazi inaendelea na tunaomba wazidi kuwa pamoja nasi.”