AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa kupoteza mchezo wao uliopita kimataifa dhidi ya Constantine kusiwatoe kwenye reli kwa kuwa malengo ni kupata ushindi katika mechi zijazo na hesabu kubwa ni kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Ipo wazi kwamba wakiwa ugenini Simba walipata bao la kuongoza dakika ya 24 kupitia kwa Mohamed Hussen, meza ilipinduliwa kipindi cha pili kwa wapinzani wao hao kufunga bao la kusawazisha na kuongeza bao la pili lililowapa pointi tatu mazima.
“Kikosi kipo salama na kupoteza mchezo wetu uliopita haikuwa malengo yetu kwani tulikuwa kwenye nafasi nzuri ya kushinda mwisho haikuwa hivyo hasa kipindi cha pili baada ya makosa ambayo yalijitokeza ndani ya dakika tano bado tuko imara na tunaendelea kupambana kupata matokeo mazuri.
“Baada ya kupoteza mchezo wetu kuna wenzetu wakaanza kukata tamaa lakini niwambie tu tuko salama sana, hakuna kilichobadilika, nafasi yetu ya kwenda robo fainali iko palepale. Niwakumbushe msimu juzi mpaka mchezo wa pili hatukuwa na alama yoyote na tukaibukia kwa Vipers na kila mmoja anakumbuka Mnyama akavuka kwenda robo fainali.
“Kupoteza na CS Constantine kusitutoe kwenye reli, nafasi yetu ya kwenda robo fainali bado nyeupe kabisa. Nafasi yetu bado iko wazi tukifanya vizuri mechi inayofata. Mchezo wa Jumapili lazima kila Mwanasimba ajue umuhimu wake maana mpinzani tunayekutana nae anataka kufufukia kwetu na sisi hatuko tayari kuona CS Sfaxien anafufukia kwetu. Hakuna ambaye amewahi kupata uhai ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa.”