KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hemed Suleiman, (Morocco) ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo unaotarajiwa kuchezwa leo Machi 25 2024 hivyo hawatakuwa tayari kupoteza kwa mara nyingine tena.
Stars itakuwa na kibarua kwenye mchezo wa FIFA Series dhidi ya Mongolia ukiwa ni mchezo wa pili baada ya ule wa awali dhidi ya Bulgaria uliochezwa Machi 22 na Stars kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Ikumbukwe kwamba Stars imeweka kambi ya wiki moja jijini Baku, Azerbaijan kwa ajili ya michezo ya FIFA Series ambapo tayari dakika 90 za awali iliambulia maumivu.
Kocha huyo amesema:”Mchezo uliopita tulishindwa kupata matokeo makosa tumeyafanyia kazi na ambacho tunaamini ni kwamba inawezekana kupata matokeo hilo lipo wazi kwa kuwa wachezaji wapo tayari,”.
Nyota Feisal Salum amesema kuwa wanatambua wana kazi ngumu ya kufanya lakini watashirikiana kupata matokeo mazuri.
“Tunaahidi ushindi kwenye mchezo wetu baada ya ule wa kwanza kupoteza, tupo tayari na benchi la ufundi linatupa maelekezo ambayo tutayafanyia kazi,”.