TAWASIFU YA WAZIRI MKUU MSTAAFU EDWARD NGOYAI LOWASSA

 

Tumsifu Yesu Kristu, Bwana Yesu Asifiwe,

Raha ya Milele umpe Eeeh Bwana, apumzike kwa Amani. Raha ya Milele umpe Eeeh Bwana, apumzike kwa Amani. Raha ya Milele umpe Eeeh Bwana, apumzike kwa Amani.

Tunaposimama hapa leo, mioyo yetu imejaa huzuni na machozi, lakini pia, imejaa shukrani na heshima kwa maisha ya kipekee ya Baba na mpendwa wetu, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa ambaye leo anahitimisha safari yake hapa duniani.

Wakati tunapomuaga Baba yetu kwa maombolezo na machungu, tunajikuta tukilazimika kumkumbuka na kusherehekea maisha yake ambayo yamekuwa darasa kubwa kwa mama yetu Regina, familia, taifa, Afrika Mashariki, Afrika na dunia.

Maisha ya baba yetu Edward Ngoyai Lowassa, ni ushahidi kwa kila aliyemfahamu vyema, kuwa alikuwa ni tunu na nyota ing’arayo, na mtu adhimu wa aina yake.

Rekodi ya kazi zake ndani ya chama, tangu akiwa kijana na mtumishi katika chama cha CCM, serikalini, na katika nafasi tofauti za kisiasa na kiutendaji, zinaweza kuth- ibitisha pasi na shaka kwamba alikuwa kiongozi mbunifu, hodari, mahiri, na mwa- namikakati asiyechoka kujifunza, kufikiri, na kutenda kwa viwango vya juu kabisa.

Kwa baba yetu Lowassa, wajibu wa msingi wa kiongozi ulikuwa ni kupigania, maen- deleo ya nchi yetu, na ustawi wa watu wake, akiweka mkazo mahsusi katika ELIMU.

Kwa mujibu wa watu mbalimbali, waliomfahamu baba yetu Lowassa, tangu akiwa mvulana kule Umasaini Monduli, wametusimulia namna nyota yake ya uongozi, ilivyoanza kung’ara tangu udogoni , alipokuwa akichangamana na watu wazima, ambao walianza kusikiliza ushauri wake katika masuala mbalimbali, hata kabla hajafikia daraja la kuwa Morani.

Karama hiyo adhimu, ndiyo ambayo aliitumia katika maisha yake yote, akiyaun- ganisha makundi mbalimbali katika kila ngazi aliyokuwapo, na hatimaye kucho- chea mabadiliko akianzia ndani ya familia yake, katika kabila lake la Wamasai hapa nchini na katika nchi jirani ya Kenya , Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Sisi kama familia tunajua, na Taifa linaweza kuthibitisha, kuwa, kama kuna mfano wa kiongozi mstaarabu, mkweli na mstahimilivu katika taifa, anayeweza akawa mfano halisi, na rejea kwa nchi yetu, aliyefundwa na viongozi waasisi wa taifa letu kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, basi, kiongozi wa namna hiyo si mwingine bali ni Edward Ngoyai Lowassa.

Kama ilivyo kwa jamii kubwa ya Watanzania waliobahatika kuvuna hekima na upendo wake usiomithilika, hata sisi wana familia yake, ambako alikuwa baba, kaka, shemeji, babu na mjomba wetu, Edward Lowassa alikuwa mwamba wa upendo, na faraja kwetu, na kwa kila mmoja wetu.

Kwa mama yetu Regina, alikuwa kichwa cha familia, mume mwema, na rafiki ambaye aliipenda familia yake kwa dhati, na kupigania maendeleo kimaisha na hususan kielimu.

Kutoka katika sakafu ya moyo wake, wakati wote, alionyesha kwa vitendo, namna alivyotamani kuiona Tanzania ikistawi kijamii na kiuchumi.

Baba yetu Lowassa, aliamini kabisa katika nukuu ya mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa, Anatole France aliyeishi karne ya 18 hadi mwanzoni mwa karne ya 19 ambaye alipata kusema; “Poverty is like Poison in the Body Politic; It Undermines the Health of the Entire Nation.”

Kwa lugha rahisi, mwanazuoni huyo alikuwa akimaanisha kwamba; “Umaskini ni kama ilivyo sumu katika mwili wa jamii, inayoleta magonjwa ya kila aina.”

Maneno hayo yanaakisi, kile ambacho Mzee wetu alikisema kwa msisitizo, na kwa kurejea mara kadhaa; “Nauchukia Umaskini”.

Hivyo basi, ndugu zangu mlioungana nasi, kuomboleza, na kusherehekea maisha ya baba yetu mpendwa, tunaomba, tumuenzi baba yetu Lowassa kwa kufanya kazi kwa bidii, na kuuchukia umaskini. Huku tukirejea salamu aliyoipenda, sana akiwa kion- gozi kwa kusema; “Hongera kwa Kazi” badala ya salamu ya kimazoea ya “Pole kwa Kazi”.

Ni kwa sababu ya kuthamini na kutambua maana ya kazi, sambamba na kusimamia imani yake kuhusu ELIMU. Baba yetu Lowassa, akiwa mbunge na baadaye Waziri Mkuu, aliliongoza taifa katika kuhimiza ujenzi wa shule za sekondari za kata, ambazo miaka michache baadaye, zikawa ndiyo kimbilio na fursa, kwa watoto wanaotoka katika familia maskini, kupata elimu.

Kama ilivyokuwa kwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela, aliyesema. “Educa- tion is the most powerful weapon, which you can use to change the world.”

Akiimanisha ; Elimu ni silaha yenye nguvu, ambayo unaweza kutumia kubadilisha ulimwengu”, ndivyo ilivyokuwa pia, kwa mwanabadiliko, baba yetu Edward Ngoyai Lowassa.

Hakuishia tu katika ujenzi wa shule za kata, kwani aliamini baada ya vijana kufaulu sekondari, walipaswa kuendelea na elimu ya juu. hivyo basi, akashiriki katika kuasi- si wazo, la kuanzisha mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), chuo ambacho leo kimekuwa kitovu kikuu cha elimu na kimbilio la maelfu ya vijana wa Kitanzania.

Hata alipokuja na wazo kwamba angetoa elimu bure ya msingi na sekondari, kama namna ya kufikia matarajio na malengo, baadhi ya viongozi wenzake wengi kutoka makundi na vyama tofauti hawakumuelewa mapema.

Kitendo cha baba yetu, kuwapa fursa ya elimu vijana, ilikuwa hatua ya kwanza ya kuelekea kuitimiza ndoto yake ya kujenga taifa imara, la wachapakazi, walioelimika, na ambao hatimaye wangelikuwa wanamapinduzi wa kwanza, wa mabadiliko na maendeleo.

Halikuwa ni jambo la kubahatisha au bahati mbaya, alipokuja na wazo la Safari ya Matumaini, kama ajenda kuu yake ya awali katika kutafuta fursa ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi, kuwa mgombea Urais mwaka 2015.

Mbegu ya fikra alizopanda katika elimu, uchumi, na kijamii , ndizo ambazo miaka kadhaa baadaye zilikuja kuchukuliwa na kufanyiwa kazi na viongozi wenzake.

Siku zote, baba alitambua kwamba vijana ni msingi wa mustakabali wa taifa kuson- ga mbele.

Hivyo basi, tuyaishi mema yake, lakini pia tukitembea katika maneno ya mwanafal- safa Plato ya kwamba, “By educating the young, we are preparing them to lead the nation.” – kwa tafsiri ya Kiswahili; kwa kuelimisha vijana, tunawaanda kuongoza taifa.”

Baba yetu Lowassa, alikuwa mtu wa mfano kwa vijana, alifanya kazi kwa bidii, uaminifu, na uwazi, na aliwahamasisha vijana kufanya vivyo hivyo. Alionyesha kwamba, uongozi si tu kuhusu kuwa na mamlaka, bali pia ni kuwa na wajibu na kuleta matumani na mabadiliko kwa jamii.

Kupitia mchango wake katika kulea vijana katika uongozi, Lowassa ameacha alama kubwa, ambayo itaendelea kuishi milele. Vijana waliopata fursa ya kufanya kazi naye au kunufaika na uongozi wake watakuwa na mengi ya kumwelezea.

Katika maisha yake, Baba ilikuwa na kawaida kuanza kazi asubuhi saa 12 na kumal- iza usiku. Alipenda sana kazi. Kwake nidhamu ya kazi halikuwa ni jambo la hiari.

Wanaokumbuka akiwa Waziri Mkuu Kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, walikuwa wakijua namna ilivyokuwa kawaida kwao kuwahi bungeni, na kuwapo katika vikao ambavyo yeye alikuwapo.

Kwake yeye baba yetu, kiongozi alipaswa kuongoza kwa mifano kama hatua ya mwanzo ya kiuwajibikaji kwake mwenyewe na kwa aliokuwa anawaongoza.

Pamoja na kwamba, baba alikuwa muumini mwaminifu wa madhehebu ya Kilu- theri, katika maisha yake hapa duniani aliheshimu imani ya kila mmoja, na alitoa ushirikano sawa kwa watu wa Madhehebu mengine, na hata wale wa imani tofauti.

Mama na sisi watoto wake wote, ni mashahidi wa namna alivyotuasa wakati wote wa maisha yake, kuishi kwa kuheshimu imani ya kila mtu.

Baba yetu Edward Lowassa tunayemuaga leo hapa, alizaliwa Agosti 26, elfu moja mia tisa na hamsini na tatu, (1953) katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto wa tatu kwa Mzee Baraka Ngoyai Lowassa.

Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka, Elfu moja mia tisa sitini na moja (1961) hadi sitini na saba (1967).

Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka, (1968) hadi (1971), kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka (1972) hadi (1973).

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka (1974) hadi (1977) na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu, na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza, kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo mwaka, (1983) hadi (1984).

Awali baada ya kumaliza chuo kikuu, alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa chama hicho kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka, (1977) hadi (1989).

Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka, (1989) hadi (1990).

Alimuoa mama yetu mpendwa Regina, na kujaaliwa kupata watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Richard, kaka zangu ambao ni Frederick na Robert, na dada zangu Pamella na Adda.

Alikuwa mbunge kwanza wa vijana kuanzia mwaka (1990) hadi (1995) kabla hajachaguliwa kwa kishindo, kuwa mbunge wa Monduli kati ya mwaka, (1995) hadi (2015).

Tangu alipoingia katika medani ya siasa kama kiongozi, alijipambanua kuwa ni kiongozi anayeamini katika kuchukua maamuzi magumu.

Katika nasaha zake kuhusu UONGOZI nje ya majukwaa ya kisiasa, baba alipenda kusisitiza namna ilivyo bora kwa kiongozi kuchukua maamuzi na kukosea, kuliko kutochukua kabisa maamuzi.

Miongoni mwa maamuzi magumu anayokumbukwa kuyachukua, ni ule wa kuanza kuyatumia maji kutoka katika Ziwa Victoria kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa yasiyopakana na ziwa hilo kinyume cha mkataba wa kimataifa unaoipa nchi ya Misri kuwa na haki hiyo kabla ya mataifa mengine.

Uamuzi huo ambao alianza kuutekeleza wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu alipokuwa Waziri wa Maji na Mifugo, ulileta mtikisiko mkubwa na hofu ya kuibuka kwa vita kati ya Tanzania na Misri.

Tofauti na wasiwasi huo, mradi huo wa matumizi ya maji ya Ziwa Victoria, leo ndiyo umekuwa mkombozi kwa mikoa mingi zaidi ukijumuisha mikoa ya Simiyu, Geita, Tabora na Singida.

Si hayo tu, alikuwa ni baba yetu Lowassa ambaye kipindi hicho ndipo alipoiongoza serikali kuvunja mkataba wa hovyo, ambao Mamlaka ya Maji Safi na Taka Dar es Salaam iliingia na kampuni ya Uingereza ya Bi Water na kuunda kampuni tanzu ya City Water.

Uamuzi huo ambao ulifuatiwa na hatua ya Bi Water, kuishitaki serikali ya Tanzania kwa kuvunja mkataba isivyo halali, ulisababisha taharuki kubwa nchini na baadhi ya watendaji na viongozi wenzake wakamvurumishia lawama kwamba, alichukua uamuzi wa kiimla, ambao ungeigharimu nchi.

Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, serikali ya Tanzania iliibuka kidedea katika kesi hiyo , iliyofunguliwa katika mahakama ya kimataifa ya mizozo ya kiuwekezaji

Kwa mara nyingine tena, akaibuka shujaa. kwa kiwango kilichosababisha Hayati, Rais Benjamin Mkapa, kumtaja kama mmoja , wa mawaziri wake wachache hodari, ambao kutokana na uhodari wao, aliwaita askari wa miavuli.

Safari ya Baba yetu, kufanya maamuzi magumu, ilirejea tena, alipokuwa Waziri Mkuu wakati wa serikali ya awamu ya nne, alipowaita wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, na kuwaelekeza kujenga majengo ya chuo kikuu kipya wakati huo cha Dodoma ambacho sasa ndio UDOM.

Huyo ndiye Edward Ngoyai Lowassa, ambaye uthubutu wake, wa kuchukua maamuzi magumu, aliufanya tena Februari mwaka 2008, alipotangaza kujiuzulu uwaziri mkuu, akifanya hivyo, kama hatua ya kutokubaliana na utaratibu uliotumi- wa na Kamati Teule ya Bunge, kumtuhumu katika sakata la Richmond, kabla ya kumuita na kumhoji , kama inavyopaswa kufanywa katika misingi ya haki, ya asili ya kusikilizwa.

Maamuzi hayo magumu , ni baadhi tu , ya hatua ambazo hatimaye , zilimwezesha kuendelea kuvuma kisiasa, na kuheshimika kama kiongozi mwenye uthubutu, mstahimilivu, na mkweli. na hivyo kumwezesha kuchukua fomu, ya kugombea urais kwanza ndani ya CCM, na baadaye kupitia UKAWA, na kusababisha mvumo ambao haujawahi kutokea.

Alikuwa ni baba yetu Edward Ngoyai Lowassa, ambaye kwa miaka zaidi ya 30 sasa, jina lake limekuwa likiandikwa kwa wino mzito, herufi kubwa na kupandisha homa, na joto kitaifa.

Baba yetu anafunga ukurasa wa kitabu chake, huku akituachia ukweli mchungu, na mkubwa kwamba, utakuwa ni mtihani mzito kujaribu kuvaa viatu vyake, maana karama alizobarikiwa. si rahisi kurithiwa na yeyote. Pengine, kila mmoja kwa sehemu yake, ataweza akachota sehemu tu ya utajiri wa maarifa, hekima, na uhodari aliojaliwa.

BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA,

JINA LA BWANA LIHIMIDIWE,

RAHA YA MILELE, UUMPE EEH BWANA APUMZIKE KWA AMANI.