>

KISA INONGA, BENCHIKHA AWACHENJIA MABOSI SIMBA

BENCHI la Ufundi la Simba, ambalo lipo chini ya Kocha Mkuu Mualgeria, Abdelhak Benchikha limezuia mauzo ya beki wao kati Mkongomani, Hennock Inonga.

Mkongomani huyo ni kati ya wachezaji wanaounda kikosi cha DR Congo, ambacho kimefuzu hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) huko nchini Ivory Coast baada ya kuwaondoa Misri katika hatua ya 16 bora kwa njia ya penalty.

Nyota huyo akiwa katika michuano hiyo, nchini Ivory Coast tetesi zinasema kuwa klabu ya RS Berkane ya chini Morocco imeonyesha nia kubwa ya kumuhitaji beki huyo anayeunda kikosi cha kwanza cha DR Congo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Benchikha amezuia beki huyo kuuzwa katika klabu yoyote huku akiuomba uongozi umuongezee mkataba mwingine wa kuendelea kubakia hapo.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa sababu ya kocha huyo, kuzuia kuuzwa kwa beki huyo ni kutokana na kuwepo katika mipango yake ya muda mrefu ya kuendelea kubakia hapo ili kufanikisha malengo yake aliyoyatoa ya kubeba makombe yote wanayoshiriki kwa kuanzia msimu huu.

“Inonga ni kati ya wachezaji waliopo katika mipango ya muda mrefu ya kocha wetu Benchikha, ambaye amezuia kuuzwa kwa beki huyo katika msimu huu.

“Hivyo hatauzwa kwenda popote katika msimu huu, badala yake ataendelea kubakia hapa Simba kutokana na kiwango chake ambacho anacho hivi sasa.

“Pia wapo wachezaji wengine ambao kocha ameshauri kutoondoka hapo, huku akishinikiza kuwaongeza mikataba mingine kwa wale inakaribia kumalizika,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia hilo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa: “Inonga yupo na ataendelea kuwepo Simba, kwani mchezaji mwenye mkataba wa kuendelea kuwepo hapa, ngumu kumuachia kwa sasa mchezaji aina ya Inonga.”