SIMBA WAJIONGEZEA MZIGO KIMATAIFA, WAO WENYEWE SABABU

SIMBA imepoteza pointi tatu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco ukiwa ni mchezo wao wa kwanza kupoteza msimu wa 2023/24 katika anga la kimataifa.

Hakuna wakumlaumu kwa kilichotokea kutokana na kushindwa kutumia nafasi walizopata pamoja na kushindwa kukaba nafasi katika dakika za lala salama.

Kazi ni nzito kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kukwama kuanza vizuri kwenye mechi tatu za mwanzo.

Katika mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia Desemba 10 kipa Ayoub Lakred aliokoa penalti iliyosababishwa na Kibu Dennis kwenye harakati za kuokoa hatari lakini mwisho hakukamilisha dakika 90 na hati safi.

Eneo la ushambuliaji likiongozwa na Jean Baleke limeinyima pointi Simba, mpaka dakika ya 60 hakuna shuti ambalo alipiga likalenga lango.

Ni Moses Phiri alikuwa wa kwanza kipiga shuti ambalo lililenga lango na mwisho ubao ukasoma Wydad Casablanca 1-0 Simba.

Mchezo ujao kwa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika unatarajiwa kuchezwa Desemba 19, Uwanja wa Mkapa ambapo Simba wanaburuza mkia wakiwa na pointi mbili.