MATAJIRI WA DAR MOTO WAO SIO WAKITOTO

MATAJIRI wa Dar Azam FC moto wa ushindi hauzimi kutokana na kuendelea pale walipoishia Novemba kupata ushindi mbele ya wapinzani wao na kukomba pointi tatu.

Ipo wazi kuwa ndani ya Novemba katika mechi tatu mfululizo, mbili ambazo ni dakika 180 walicheza ugenini na kete ya kufungia mwezi ikipigwa Azam Complex zote waliibuka na ushindi.

Katika mechi tatu safu ya ushambuliaji ya Azam FC ilifunga jumla ya mabao 11 huku ukuta ukiruhusu bao moja pekee ugenini. Ilikuwa Novemba Mosi ubao wa Uwanja wa Lake Tanganyika ulisoma Mashujaa 0-3 Azam FC

Novemba 4 ubao wa Uwanja wa Highland Estate ulisoma Ihefu 1-3 Azam FC, ukiwa ni mchezo wa kwanza ndani ya Novemba kufungwa ikiwa ugenini.

Novemba 24 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Azam FC 5-0 Mtibwa Sugar hii ilikuwa kete ya tatu kufunga Novemba wakikamilisha dakika 270 ndani ya Novemba.

Kete ya kwanza kufungulia Desemba walikuwa nyumbani ubao wa Uwanja wa Azam Complex Desemba 7 ulisoma Azam FC 5-0 KMC.

Hivyo moto wa Azam FC kwenye mechi nne ambazo ni dakika 360 haujazima, wakikomba pointi 12 safu ya ushambuliaji ikitupia mabao 16 ikiwa na hatari wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 22.

Kinara wa utupiaji ndani ya Azam FC yenye muuaji anayetabasamu Prince Dube ni Feisal mwenye mabao 7 kibindoni akiwa na pasi nne za mabao ndani ya Azam FC ambao ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 11.

Ikumbukwe kwamba kiungo Feisal Salum Novemba alitwaa tuzo ya mchezaji bora ndani ya ligi akiwapoteza Maxi Nzengeli wa Yanga na Kipre Junior wa Azam FC.

Mbali na Feisal pia kocha wake Bruno Ferry naye alitwaa tuzo ya kocha bora wa mwezi akiwapiku Miguel Gamondi wa Yanga na Heron Ricardo wa Singida Fountain Gate.