HUZUNI kwa mashabiki kushindwa kupata kicheko kwenye mechi za kimataifa inapaswa kuondolewa na wachezaji uwanjani.
Hali haijawa nzuri kwenye mechi za kimataifa ambapo ni timu mbili kutoka ardhi ya Tanzania zinafanya kazi yake. Yanga na Simba katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kila timu ikiwa imecheza mechi mbili hakuna iliyoambulia ushindi jambo linaloongoza huzuni kwa mashabiki na wachezaji wenyewe kupoteza ile hali ya kujiamini.
Ushindi ni mzuri na unaleta tabasamu kwa kila pande hasa kwa mashabiki wa timu hizi mbili ambazo zina kazi kubwa kufanya kwenye mechi za kimataifa hatua ya makundi.
Inawezekana kupata matokeo mazuri ikiwa wachezaji watafanya kazi kubwa kutumia makosa ambayo yanafanywa na wapinzani na wao pia wakapunguza makosa kwenye mechi ambazo wanacheza.
Ni sasa wachezaji kuamua kujituma kwa kuwa kucheza wanajua na uwezo wanao kilichobaki ni kupata matokeo ambayo yanakosekana kwenye mechi hizi za mwanzo.
Ikiwa mwendelezo utakuwa hivi kuna uwezekano mkubwa wawakilishi wote wa Tanzania kugotea hatua ya makundi jambo ambalo halitakuwa ni matokeo mazuri kwetu.
Kila mchezaji ni muhimu kutambua kwamba kazi ya kimataifa inahitaji kujitoa kwa kila wakati bila kukata tamaa na kushirikiana katika kutafuta matokeo.
Kila la kheri kwenye mechi ambazo zipo mbele iwe ni ugenini ama nyumbani, muda wa kuondoa huzuni ni sasa na kicheko kitawale kwa mashabiki.