KAZI KIMATAIFA LEO HAKUNA MWENYE SHUGHULI NDOGO

    HATIMAYE imefika siku ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki pamoja na benchi la ufundi kuona kipi kitapatikana ndani ya dakika 90.

    Ligi ya Mabingwa Afrika, mashindano yenye ushindani mkubwa yanatarajiwa kuendelea leo na wawakilishi wa Tanzania, Simba na Yanga watakuwa kazini.

    Yanga watakuwa nyumbani Uwanja wa Mkapa huku Simba wakiwa ugenini, Botswana wote kazi ni moja kusaka pointi tatu kwenye mechi za kimataifa.

    Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika Al Ahly watakuwa kwenye Uwanja wa Mkapa kusaka pointi tatu dhidi ya Yanga. Simba watakuwa na kazi ya kusaka ushindi dhidi ya Jwaneng Galaxy.

    Hakuna mwenye kazi nyepesi kwa kuwa kila timu inapambana kusaka pointi tatu kwenye mechi husika. Hivyo mashabiki wanapaswa kutambua kwamba dakika 90 zina matokeo kamili na sio kuanza kujipa matumaini timu itashinda.

    Porojo na hamasa kwenye sayansi ya mpira ni vitu viwili tofauti hivyo maneno yanazungumzwa ni kuyasikiliza na kuamini kwamba licha ya yote haya dakika 90 zitaamua nani atakuwa mshindi.

    Wachezaji wanatambua hakuna ushindi bila ya kufunga mabao na kulinda hayo mabao. Kazi iwe moja kwa wawakilishi hawa wa Tanzania kusaka ushindi bila kuogopa.

    Furaha ya mashabiki ni kuona timu inashinda na furaha ya benchi la ufundi ni kushuhudia wachezaji wanatimiza majukumu kwa umakini.

    Ni sasa kufanya kweli na inawezekana nyumbani ama ugenini, kila la kheri wawakilishi wa Tanzania kimataifa.

    Previous articleAZAM FC YAFUNGA NOVEMBA KIBABE
    Next articleNYUMBANI TUNAPIGA, UGENINI TUNACHINJA