Home Entertainment BODI YA FILAMU YAKAMILISHA MCHUJO TUZO 2023

BODI YA FILAMU YAKAMILISHA MCHUJO TUZO 2023

BODI ya Filamu Tanzania imekamilisha mchujo wa pili wa filamu ambazo zitakwenda kushindaniwa katika kupata washindi wa Tamasha la tuzo za Filamu kwa mwaka 2023.

Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msingwa alisema kuwa Tuzo za Filamu Tanzania zimechochea uanzishwaji wa tuzo nyingine hapa nchini, ikiwemo zile za wadau kupitia vyama ambavyo wamevianzishwa mikoani kwa ngazi za mikoa.

“Kwa wadau mnaoandaa matamasha na tuzo za Filamu hapa nchini, niwakumbushe kupata vibali kutoka Bodi ya Filamu vya kuandaa matasha hayo pamoja na tuzo hizo kama ilivyoelekezwa kwenye kanuni ya Filamu na Michezo ya kuigiza za mwaka 2020, pamoja na muongozo wa uendeshaji matamasha ya Filamu na Michezo ya kuigiza iliyoandaliwa na bodi ya Filamu.

Nichukue nafasi hii, kuwakumbusha kuzingatia taratibu,kanuni na sheria zinaongoza Filamu na Michezo ya kuigiza Nchini pale mnapofanya shughuli zenu za kuigiza kwa kuhakikisha mnapata vitambulisho vya kuwatambulisha kuwa mnajishughilisha na shughuli za Filamu,” alisema Msingwa.

Nae Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt.Kiagho Kilonzo amesema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kufanya tathmini kila wanapomaliza msimu mmoja wa tuzo kuona ni kwa kiasi gani nia hiyo njema ya Serikali inafikiwa .

“Mara zote tathmini zetu zinaonyesha kuwa Tuzo hizi za Serikali zimesaidia sana kutangaza sekta ya Filamu ndani na nje ya Nchi, zimeibua vipaji vilivyojificha, Zimeongeza ubora wa filamu zinazozalishwa hapa Nchini na zimeibua fursa nyingi za uwekezaji na mashirikiano kwenye eneo hili la Filamu,” amesema Kilonzo.

Previous articleMWANZO MBAYA KIMATAIFA IWE NI SOMO KWA VITENDO
Next articleBOSI SIMBA AMEFUNGUKA MWENDO WA TIMU NA UGUMU ULIOPO