KIEPE NYANI, TANZANIA ONE ASIYEIMBWA

FADHILI Majiha (Kiepe Nyani) bondia wa ngumi za kulipwa nchini ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa bondia namba moja (Tanzania One) akiwa na hadhi ya nyota nne.

Majiha ambaye ni bingwa wa WBC Afrika na UBO alianza kucheza ngumi za kulipwa mwaka 2008 ambapo pambano lake la kwanza alipanda ulingoni dhidi ya Ramadhan Kumbele ambalo alifanikiwa kushinda kwa pointi katika pambano lililofanyika kwenye Ukumbi wa Traveltime, Dar.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 50 akiwa ameshinda 32 kati ya hayo 15 ni kwa KO na amepoteza 14, matatu yakiwa ni kwa KO  na ametoka sare mara nne.

Licha ya kutoimbwa na mashabiki wengi wa mchezo huo lakini Majiha ni bondia anayeshikilia rekodi ya kushinda mikanda miwili ya ubingwa wa WBA Pan-African nje ya taifa la Tanzania na kushinda mapambano mengine mawili nje ya mipaka ya Tanzania.

Mwaka 2011 alienda nchini Uganda kucheza pambano lake la kwanza la kimataifa kuwania mkanda wa ubingwa wa Dunia wa UBO dhidi ya Mude Ntambi lakini alipoteza kwa pointi katika pambano la raundi 12.

Lakini mwaka, 2013, Majiha aliweka rekodi ya kushinda pambano lake la kwanza nje ya mipaka ya Tanzania kwa kumchapa kwa pointi Heri Amol wa Indonesia akiwa kwenye ardhi yao.

Majiha hakuishia hapo kwani mwaka 2017, Mtanzania huyo aliweka rekodi ya kushinda mkanda wa kwanza wa ubingwa wa WBA Pan-African dhidi ya Gabriel Ochieng katika pambano lilipigwa jijini Nairobi nchini Kenya huku akishinda kwa ushindi wa pointi katika pambano la raundi 12.

Rekodi ya kutoa vichapo vya ubingwa akaendeleza tena, mwaka 2018 kwa kushinda tena mkanda wa WBA Pan-African dhidi ya Rofhwa Nemushungwa wa Afrika Kusini tena akiwa kwenye ardhi ya kwao Afrika Kusini.

Mwaka 2021, Majiha ameweka rekodi nchini Uingereza kwa kumchapa kwa TKO ya raundi ya nne katika pambano la raundi kumi Harvey Horn  kabla ya mwaka huu kushinda ubingwa wa UBO, Mwanza kwa kumbutua Rent Rosia kwa pointi kisha akamaliza kwa kumchapa Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini na kushinda ubingwa wa WBC Afrika.

Kwa sasa yeye ni bondia namba moja Tanzania akiwa na rekodi ya nyota nne na nusu ambazo hazijawahi kufikiwa na bondia yoyote nchini huku Duniani akiwa anakamata nafasi saba katika mabondia 1,051 wa uzani wake.

Majiha au Kiepe Nyani kama anavyoitwa na mashabiki wengi baada ya kumpiga Mghana anasema kuwa amewahi kuitwa Mghana kutokana na rekodi yake yakuwapiga wengi jambo ambalo lilimuumiza na kumkatisha tamaa.

“Nishaitwa hadi Mghana, nilikata tamaa lakini kwamba wakati wa Mungu ndiyo wakati sahihi kutokana na sasa kufikia kwenye daraja langu.

“Mipango yangu kwa sasa nikucheza na mabondia ambao wemenizidi rekodi na siyo hawa ndani kwa sababu hawana uwezo wa kunisumbua, nashukuru kwa sasa pia nimeanza kupewa heshima yangu, ” anasema Majiha.