KIVUMBI LIGI DARAJA TATU PWANI KINAKUJA

KIVUMBI cha Ligi daraja la tatu kwa mkoa wa Pwani kinatarajiwa kuanza Novemba 4 2023 katika makundi mawili tofauti ambapo jumla ya timu 14 zitashiriki.

Ligi hiyo ya Daraja la tatu ngazi ya mkoa inasimamiwa na Chama Cha Soka mkoa wa Pwani (COREFA) ambapo itachezwa kwa mfumo wa Kanda katika mkoa ikiwepo Kanda ya Kusini na Kaskazini.

COREFA chini ya Mwenyekiti Robart Munis imelazimika kupanga utaratibu huo wa kanda katika michezo hiyo kutokana na jiografia ya mkoa wa Pwani ilivyo ukilinganisha na uwezo wa vilabu shiriki katika michezo hiyo.

taarifa ambayo imetolewa leo  Novemba Mosi 2023 na Christina Mwagala, Meneja wa Habari na Mawasiliano COREFA imeeleza namna hii:-

“Ukiangalia Kanda ya kusini inahusisha Wilaya ya Mkuranga, Rufiji, Kibiti pamoja na Mafia, upande wa Kaskazini inahusisha Wilaya ya Kibaha, Bagamoyo pamoja na Kisarawe.

“Kwahiyo kunakuwa na changamoto za ki jiographia kutoka sehemu na sehemu hivyo kufanya vilabu visiweze kuhimili gharama ndio mana tukaweka kwenye mfumo wa kikanda.

“Hata hivyo katika hatua nyingine kamati ya ufundi imejiridhisha na viwanja vyote ambavyo vinatumika katika michezo hiyo ya Ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa wa Pwani,”.