Home Sports FUPA LILILOMSHINDA MTANI, MIKONONI MWA MNYAMA

FUPA LILILOMSHINDA MTANI, MIKONONI MWA MNYAMA

MBINU za makocha wawili zitakuwa kazini leo kusaka pointi tatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Mkapa. Ni Roberto Oliveira wa Simba dhidi ya Moses Basena wa Ihefu.

Oliveira ameliambia amesema kuwa wanahitaji pointi tatu kama ambavyo Basena mrithi wa mikoba ya Zuber Katwila naye anahitaji kuona wakikomba pointi hizo muhimu.

Hapa tunakuletea namna ngoma inavyotarajiwa kupigwa taratibu namna hii:-

Ugonjwa wa Clean Sheet kuendelea?

Ukuta wa Simba kwenye mechi tano za mashindano mfululizo walizocheza hakuna clean sheet, (cheza bila kufungwa) ndani ya dakika 450 walitunguliwa mabao sita.

Mchezo wa leo utakuwa ni mchezo wa sita ambapo safu ya ulinzi ikiongozwa na Henock Inonga itakuwa na kazi ya kujiuliza namna gani watapata dawa ya ugonjwa huo unaowatesa wakiwa kwenye mechi za ushindani.

Langoni kivumbi

Lango la Simba bado linajitafuta kwa sasa kutokana na maumivu aliyoyapata Aishi Manula. Licha ya kupona nafasi ya kuanza kwenye mchezo wa leo ni ndogo.

Yupo Ayoub Lakred ingizo jipya ndani ya Simba kwenye mechi zilizopita alianzia benchi. Ally Salim bado hajawa imara langoni kutokana na makosa anayofanya katika kupangua mipira hivyo benchi la ufundi upande wa makipa linapambania kombe kuwarejesha kwenye ubora.

Ihefu wao yupo Fikirini Bakari ambaye alianza kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga, Mbeya.

Vita ya ufungaji bora

Jean Baleke nyota wa Simba anatambua ushindani uliopo kwenye kasi ya upachikaji wa mabao. Hatakuwa mnyonge akipewa nafasi ya kuanza katika mchezo wa leo dhidi ya Ihefu.

Mabao yake matano kibindoni baada ya Simba kucheza mechi tano yanampa nguvu ya kuendelea pale ambapo aliishia. Mara ya mwisho kufunga ilikuwa kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union. Kwenye mchezo huo alifunga hat trick na Simba ilikomba pointi tatu mazima.

Ni Aziz Ki wa Yanga katupia kambani mabao sita na Feisal Salum wa Azam FC huyu kibindoni alikuwa na mabao manne hawa walikuwa ndani ya tatu bora.

Mfupa mgumu kwa Yanga

Kwa msimu wa 2023/24 Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ilikuwa na rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo ambazo ni dakika 270 walipata ushindi.

Joto ya kupoteza pointi walikutana nayo walipofika Mbeya. Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Highland Estate ulisoma Ihefu 2-1 Yanga ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kupoteza.

Ikumbukwe kwamba Ihefu ni fupa gumu kwa watani za jadi wa Simba hivyo kazi haitakuwa nyepesi kwenye msako wa pointi tatu. Simba ni mechi tano walicheza bado hawajapoteza.

Mbio za ubingwa

Bado ligi ipo mzunguko wa kwanza kila timu ina nafasi ya kufikia malengo ya kutwaa ubingwa. Ikiwa Simba itapoteza mchezo wa leo utakuwa mchezo wake wa kwanza kuonja ladha ya kukosa pointi tatu huku ikianza kupunguza kasi ya ushindi.

Ihefu watazidi kuongeza nguvu kwenye mtaji wao wa pointi ndani ya ligi.

Ukuta wa kazi

Ihefu wana ukuta wa kazi ukiwa na miamba yenye migumu. Juma Nyoso mkongwe wa kazi yupo ndani ya kikosi cha Ihefu.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka na kutoka gazeti la Championi Jumamosi.

 

Previous articleUSHINDI MKONONI MWAKO NA KASINO YA MTANDAONI
Next articleCIRCUS FEVER DELUXE SLOTI YA UTAJIRI