MZIZIMA DABI, ATAKAYEMFUNGA PAKA KENGELE KUJULIKANA

    MZIZIMA Dabi Yanga dhidi ya Azam FC ipo jikoni inapikwa kwa sasa kabla ya kuwekwa mezani kwa wababe hao kuanza msako wa pointi tatu ndani ya Uwanja wa Mkapa.

    Oktoba 23, 2023 mchezo huo unatarajiwa kuchezwa huku shauku ikiwa ni nani atakayeibuka mbabe kwa kumfunga paka kengele ndani ya dakika 90.

    Hapa  tunakuletea namna timu hizo mbili mwendo wao kwenye ligi msimu wa 2023/24 namna hii:-

    Langoni

    Kwenye lango kazi kubwa inatarajiwa kuwa kwa wababe wawili ambao rekodi zao zinakwenda sawa ndani ya ligi katika idadi ya mechi amazo hawajafungwa.

    Djigui Diarra huyu ni kipa namba moja wa Yanga akiwa hajafungwa kwenye mechi tatu na ni mechi nne alikaa langoni nyota huyo akikomba dakika 360.

    Kafungwa mabao mawili ilikuwa kwenye mchezo mmoja dhidi ya Ihefu, Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.

    Idrisu Abdulai kwenye lango la Azam FC yeye ni kipa namba moja akiwa kacheza mechi zote tano akikomba dakika 450. Mabao mawili katunguliwa kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate na ule dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa mwendo wa mojamoja. Hajafungwa kwenye mechi tatu.

    Ulinzi

    Uzani upo sawa kwenye ulinzi wa timu zote mbili kutokana na idadi ya mabao ambayo walitunguliwa kuwa sasa. Timu zote zimetunguliwa mabao mawili zikicheza mechi ngumu na ushindani mkubwa.

    Yanga ukuta wake unaongozwa na Dickson Job ambaye ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi cha Yanga alifunga kwenye mchezo dhidi ya KMC.

    Ukuta wa Azam FC unaongozwa na mwamba Daniel Amoah ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Yusuph Dabo kwenye mechi zote zilizopita msimu huu alianza kikosi cha kwanza.

    Ushambuliaji

    Yanga ni namba moja kwenye safu kali yenye mabao mengi kibindoni ikiwa na mabao 15 ndani ya dakika 450 ilizocheza. Kasi kubwa kwenye viungo hawa ni wataalamu wa kucheka na nyavu ikiwa ni Maxi Nzengeli, Aziz KI, Pacome Zouzoah hawa wote wamecheka na nyavu mara tatu tatu.

    Azam FC safu yao ya ushambuliaji kibindoni ina mabao 10 kwenye dakika 450. Kinara wa utupiaji ni Feisal Salum ambaye katupia mabao manne.

    Huyu ni mfungaji wa kwanza ndani ya Azam FC alifunga mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United alipofungua ukurasa wa hat trick ndani ya msimu wa 2023/24.

    Nafasi

    Azam FC pointi zao kibindoni ni 13 nafasi yake ni ya pili huku Yanga wao pointi ni 12 nafasi ya tatu kwenye msimamo.

    Tofauti yao ni pointi moja hivyo kila timu hesabu ni kukomba pointi tatu zitakazoipelekea kwenye nafasi ya juu.

    Zali la ushindi

    Azam FC wamepata zali la ushindi kwenye mechi nne sawa na Yanga. Tofauti yao ni kwenye mechi za kupoteza na kuambulia sare. Azam FC ina sare moja huku Yanga ikiwa haijaambulia sare. Yanga ilipoteza mchezo mmoja huku Azam FC ikiwa bado haijaambulia kichapo.

    Kazi ipo kwa wababe hawa kila mmoja kutibua zali la mwenzake ndani ya uwanja.

    Tatu bora

    Ni msako wa pointi ndani ya tatu bora, Azam FC na Yanga zinaishi hapo huku kinara akiwa ni Simba mwenye pointi 15. Tofauti ya pointi mbili na Azam FC, tofauti ya pointi mbili na Yanga.

    Mshindi atapata zali la kumshusha Simba hapo kwa namna yoyote, Yanga idadi ya mabao ya kufunga ni mengi kuliko Simba, Azam FC atampoteza Simba kwa pointi ni jambo la kusubiri.

    Previous articleFEI TOTO ANA BALAA HUYO
    Next articleUtajiri Leo Hii Upo Meridianbet Bashiri Sasa