MTAMBO wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga, Maxi Nzengeli amepiga mkwara kwa kuweka wazi kuwa kazi itaonekana zaidi kwa vitendo uwanjani katika kusaka ushindi.
Nyota huyo anayevaa jezi namba 7 kibindoni katupia mabao matatu katika mechi za ligi pekee na katengeneza pasi moja ya bao ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya KMC, Uwanja wa Azam Complex.
Mabao yake kazitungua timu mbili ilikuwa ni dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa Azam Complex aliwatungua mabao mawili na bao moja aliwatungua Geita Gold, Uwanja wa CCM Kirumba.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, dozi yake alitoa ya mabao mawili alipowatungua ASAS FC dakika ya 7 na dakika ya 90 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Maxi amesema: “Ambacho tunafikiria ni ushindi kwenye mechi zetu na kupata matokeo mazuri tuwapo uwanjani. Nina amini kwamba benchi la ufundi linatupa mbinu nzuri ambazo zinatupa matokeo kwenye mechi ambazo tunacheza, tutazidi kupambana zaidi kila mechi,” .