>

MWAMBA HUYU SIMBA KUWAPA TABU KWELIKWELI

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa nyota wao Fabrince Ngoma bado anajitafuta licha ya kuonyesha uwezo kwenye mechi za ligi ambazo alipata nafasi ya kucheza.

Chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ni mechi tatu kacheza akikomba dakika 225, katupia bao moja ilikuwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Manungu.

Wachezaji wa Simba, Oktoba Mosi wana kibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Uwanja wa Azam Complex.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameliambia Championi Jumatatu kuwa uwezo wa Ngoma ni mkubwa akiwa uwanjani kile anachokifanya kwa sasa ni mwanzo kabla tu atawapa tabu sana wapinzani.

“Ameanza kuwa na mwendo mzuri na tumefurahi kuona Fabrince Ngoma anatoa pasi elekezi ambazo zinafika kwa mtu husika ni mchezaji mwenye uwezo wa kukaba na ana uwezo wa kushambulia anatoa mashambulizi na anatoa pasi za mwisho.

“Bado Ngoma bado ngoma itakuwa Oktoba 20 kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly hapo mtamuona mwenyewe eneo la kati akionyesha makeke makubwa hizi ni kazi anazozipenda.

“Ni mchezaji ambaye hapendi kupoteza pasi anazotoa akiwa uwanjani kwa kuwa huwa zinakuwa na maelekezo muhimu kwa wachezaji wenzake, tusubiri na tuone Wanasimba mazuri yanakuja,” alisema Ally.