>

SINGIDA FOUNTAIN GATE KIMATAIFA WAONGEZEWA NGUVU

WAKIWA katika maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future, Singida Fountain Gate kutoka Tanzania wameongezewa nguvu kupitia viongozi waliofika kambini.

Wawakilishi hao kwenye anga la kimataifa Oktoba Mosi watakuwa na kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya Future.

Septemba 28, 2023 ugeni kutoka kwa viongozi ikiwa ni pamoja na waziri mwenye dhamana ya michezo, Damas Ndumbaro, Balozi wa Tanzania nchini Misri, Dkt Emmanuel Nchimbi na Rais wa TFF, Wallace Karia, walifika kambini Cairo Misri na kuzungumza na wachezaji, Benchi la Ufundi pamoja na viongozi wa timu.

Viongozi hao wameongeza nguvu ya kujiamini na kuongeza hamasa ya mchezo huo wa Jumapili dhidi ya Future FC ambao ni mchezo muhimu wa kufuzu kwenda hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).

“Jisikieni mpo nyumbani. Ubalozi wenu hapa upo karibu na ninyi kwa kila hatua msiwe na wasiwasi. Sisi tunatamani kuona mnapata ushindi ili tujivunie. Tunawaamini,” amesema Balozi Nchimbi.

“Tanzania sasa ni zamu yetu. Singida ni zamu yetu. Serikali iko pamoja nanyi katika hatua hii muhimu. Kumbukeni mnaiwakilisha nchi kwahiyo msikubali kutolewa mchezoni kirahisi maana mechi kama hizi zina mambo mengi. Tunawatakia kila la kheri,” amesema  Waziri Ndumbaro.

“Hongereni sana kwa hatua hii mliyofika mpaka sasa. Tunawaombea mfanye vizuri na kwenda hatua ya makundi. TFF tutaendelea kuwapa ushirikiano wote mtakaohitaji,” amesema Wallace Karia.