BALEKE KWENYE KIVULI CHAKE NDANI YA SIMBA

MGANDAMIZO wakati mwingine hutoa kitu halisi na muda mwingine huwa kinakuwa na mvurugano kutokana na aina ya mwanga ambao utakuwa unahusika.

Kwenye Ligi Kuu Bara ndani ya Simba kuna mshamuliaji aliyefunga mzunguko wa pili 2022/23 kwa kasi kisha kaanza kuishi kwenye kivuli chake msimu wa 2023/24.

Hapa kwenye mwendo wa data tupo na nyota Jean Baleke namna hii:-

Hizi hapa kazitungua

Ni mechi tatu za ligi kapata nafasi ya kucheza akifunga kwenye kila mchezo ambao alipata nafasi ya kuanza ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji hizi ilikuwa mwendo wa mojamoja na Coastal Union aliitungua mabao matatu.

Msimu wa 2022/23 ni mabao nane alitupia kibindoni baada ya kucheza mechi 9 hivyo ni mabao matatu anadaiwa ili kuvunja rekodi yake ambayo aliiandika akiwa ardhi ya Bongo raia huyo wa Dr Congo.

Dodoma na Mtibwa kwenye zali

 Jean Baleke ana zali na Uwanja wa Manungu kwa kuwa msimu wa 2022/23 walipokutana na Mtibwa Sugar, aliwatungua mabao matatu ikiwa ni hat trick yake ya kwanza na msimu wa 2023/24 aliwatungua bao moja na timu ya Simba ilikomba pointi tatu.

Msimu huu Mtibwa Sugar ilikuwa timu yake ya kwanza kuifunga kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Manungu ilikuwa dakika ya tano.

Kwa msimu wa 2022/23 timu ya kwanza kuifunga ilikuwa ni Dodoma Jiji kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na ubao ulisoma Dodoma Jiji 0-1 Simba.

Bao la Baleke lilizama kimiani dakika ya 45 akitumia pasi ya mshikaji wake Kibu Dennis.

Dakika zake

Kwenye mechi tatu ambazo kacheza kasepa na dakika 196. Mabao yake yote matano katupia akiwa ndani ya 18.

Rekodi zinaonyesha kuwa hata msimu wa 2022/23 mabao yake yote 8 aliyofunga kwenye ligi alikuwa ndani ya 18 na alikomba dakika 616.

Mguu wake wenye nguvu

Katika mabao matano ambayo kayajaza kimiani ni mabao manne kayafunga kwa mguu wa kulia na bao moja ni mguu wake wa kushoto.

Kaifikia rekodi yake ya msimu uliopita kwenye upande wa mguu wa kulia alipofunga mabao manne huku ule wa kushoto ni mabao matatu alipachika kimiani huku bao moja ikiwa ni kwa pigo la kichwa.

Kipindi cha kwanza anawaka

Mabao ya Baleke aliyofunga ni kipindi cha kwanza anawaka. Kamba zote tano alizonazo kibindoni ilikuwa ni pale alipopewa nafasi kuanza kipindi cha kwanza kwa msimu huu wa 2023/24.

Msimu wa 2022/23 ni mabao sita alitupia kimiani alipoanza huku kipindi cha pili akitupia mabao mawili akagotea kwenye mabao nane kibindoni.