AFYA YA WACHEZAJI NI MUHIMU, WACHEZAJI LINDANENI

KAZI kubwa kwenye Ligi Kuu Bara imezidi kuonekana ambapo wachezaji wameonekana wakifanya kweli kwenye kutimiza majukumu yao.

Hili ni muhimu kuendelea kwenye kila mchezo jambo ambalo litaongeza umakini kwenye msako wa pointi tatu. Tunaona namna ambavyo kila timu inapambana kutimiza majukumu yake.

Kwa wachezaji jukumu lenu ambalo mmepewa ni kutafuta ushindi na suala la kuumizana kwenye mchezo hilo sio sawa kwa kuwa hakuna ambaye kapewa majukumu hayo.

Inatokea bahati mbaya kwa wachezaji kugongana uwanjani lakini kuna umuhimu wa kuacha kutumia nguvu nyingi sehemu ambayo haipaswi kuwa hivyo.

Wachezaji wengi wanakwama kukamilisha dakika 90 na kuingia kwenye kupambania hali zao ikiwa ni mwanzo wa msimu.

Hili linapaswa kuongezewa umakini kwa wachezaji wote kila wanapoingia uwanjani ili kuongeza ushindani na sio hofu ya kuhofia wachezaji kupata maumivu.

Sio Ligi Kuu Bara pekee mpaka Championship, Ligi ya Wanawake Tanzania ni muhimu kila mchezaji kuwa mlinzi wa mchezaji mwenzake.

Mchezo wa mpira sio vita bali ni kazi ambayo inafuatiliwa na familia kubwa duniani hivyo kuumizana sio jambo jema katika mechi za ushindani hata zile za kirafiki pia.

Maandalizi mazuri yanahitajika kwenye mechi zote na umakini kwenye kutafuta ushindi ni jambo la umuhimu kwa kuwa afya ya mchezaji ni bora kuliko kumchezea faulo.