NBC YAZINDUA NEMBO MPYA YA CHAMPIONSHIP

NI Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Septemba 7 imezindua rasmi chapa mpya ya Ligi ya Daraja la Kwanza (championship).

Ligi hiyo kwa sasa inafahamika kwa jina la NBC Championship hatua ambayo imekwenda sambamba na uzinduzi wa mashindano hayo ya soka yanayotarajiwa kuanza Septemba 9.

Ujio wa chapa hii ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa udhamini uliosainiwa hivi karibuni baina TFF unaotoa fursa ya kuendelea na udhamini wa kwenye ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara ‘NBC Premier League’ hadi msimu wa 2027/28.

Mkataba huo una thamani ya TZS 32.56 bilioni pia unajumuisha ligi za vijana kwa klabu zinazoshiriki ligi kuu ‘NBC Youth League’ na ligi ya daraja la kwanza “NBC Championship”.

Tukio la uzinduaji wa chapa hii mpya umefanyika Makao Makuu ya NBC jijini Dar na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo wakiwemo viongozi waandamizi na wadau wengine wa mchezo wa mpira wa miguu wakiwemo waandishi na wachambuzi.