Home Sports MKWARA MZITO SIMBA IMETOA KIMATAIFA

MKWARA MZITO SIMBA IMETOA KIMATAIFA

HUKU droo ya mashindano maalum ya African
Super League ikitarajiwa kupangwa rasmi leo
Jumamosi, wawakilishi wa Tanzania katika
mashindano hayo, Simba wamechimba mkwara
mzito kwa kuweka wazi wamesuka mkakati
mzito wa kuhakikisha wanapambania kushinda
ubingwa wa mashindano hayo.

Kuendana na waratibu wa mashindano hayo
yanayotarajiwa kupigwa mwezi Oktoba,
imethibitishwa yanatarajiwa kushirikisha timu
za Petro de Luanda (Angola), TP Mazembe
(DRC), Al Ahly (Misri), Horoya (Guinea), Wydad
Casablanca (Morocco), Simba (Tanzania),
Esperance (Tunisia) na Mamelodi Sundowns ya
Afrika Kusini huku kukiwa na uwezekano wa
kukutana na Mamelodi, Esperance au Wydad.

Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika kwa
mara ya kwanza barani Afrika na yanatajwa
kuwa mashindano ghali zaidi ambapo bingwa
anakadiriwa kuvuna kiasi cha zaidi ya Dola za
Marekani Milioni 11.6, sawa na zaidi ya Shilingi
Bilioni 29.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba,
Salim Abdallah; amesema: “Tulikuwa
tunaulizwa ni kwa nini tumefanya usajili
mkubwa sana kupitia dirisha kubwa la usajili
mwaka huu na ukweli ni kwamba miongoni
mwa sababu kubwa ni ushiriki wetu wa
mashindano ya Super League.

“Tuna uzoefu mkubwa na mashindano ya
kimataifa na tunakwenda kukutana na timu
kubwa Afrika, lakini hatutaki kwenda kushiriki tu tunataka kuwa miongoni mwa timu
zitakazoshinda ubingwa wa mashindano haya.

“Tuna kikosi bora na imara cha wachezaji wengi
wenye uzoefu hivyo, ni matumaini yetu kuwa
tutafanya makubwa na kuendelea kuiwakilisha
nchi vyema katika mashindano ya kimataifa,”.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua
vumbi Oktoba 20, mwaka huu katika Uwanja
wa Mkapa, Dar kwa kuanzia hatua ya robo
fainali ambapo mechi zitakuwa zinachezwa kwa
mtindo wa mtoano na michuano hiyo itadumu
kwa wiki nne.

Fainali ya michuano hiyo ambayo zitakuwa
mbili itapigwa Novemba 5, huku ile ya pili ikiwa
Novemba 11.

Previous articleAIR MANULA AREJEA UWANJANI BAADA YA KUWA NJE KWA MUDA
Next articleMASTAA YANGA WAPIGWA STOP NA GAMONDI