>

SIMBA INASUKWA UPYA KITAIFA NA KIMATAIFA

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa muda uliopo kwa sasa ni benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kusuka silaha za maangamizi kwenye mashindano ya kimataifa.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ina pointi sita kibindoni baada ya kucheza mechi mbili huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao sita na ile ya ulinzi imefungwa mabao manne.

Vinara wa ligi ni Yanga wakiwa wamecheza mechi mbili na kushinda zote huku safu ya ushambuliaji ikitupia mabao 10.

Mtupiaji wa kwanza ndani ya Yanga ni beki Dickson Job na mtupiaji wa kwanza ndani ya Simba ni Jean Baleke.

 Mchezo wao ujao kimataifa hatua ya pili Ligi ya Mabingwa ni dhidi ya Power Dynamo unaotarajiwa kuchezwa Septemba 16 Uwanja Levy Mwanawasa, Zambia.

 Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa hesabu kubwa kwa wakati huu ni kufanya maandalizi mazuri kwenye mechi za kimataifa.

“Silaha za ushindi kwenye mechi za kimataifa lazima ziandaliwe vizuri na unajua kwamba ili kupata ushindi lazima wachezaji wawe tayari na hilo wanalitambua hatuna mashaka.

“Kila kitu tunaamini kitakuwa sawa wapinzani wetu tunatambua wanajua wanakutana na timu ya aina gani. Inapofikia hatua ya mechi za kimataifa hilo ni suala kubwa na tunawaheshimu wapinzani wetu ila ambacho tunafanya ni kuwa tayari,” amesema Ally.