Home Sports SHEREHE KWA YANGA KISA KUWAFUNGA ASAS INATOSHA

SHEREHE KWA YANGA KISA KUWAFUNGA ASAS INATOSHA

USHINDI wa kwanza, Yanga wakiwa (ugenini), walifanikiwa kushinda kwa mabao 2-0 na waliporejea wakawatwanga kwa mabao 5-1.

Ushindi huo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, unaifanya Yanga kuvuka hadi hatua ya kwanza ikiwa inakwenda kukutana na El Merreikh ya Sudan.

Mechi ya Yanga dhidi ya ASAS FC bila shaka haikuwa mechi ya kumpa hofu Mwanayanga au mpenda mpira yoyote wa Tanzania. Zaidi ilikuwa ni kukumbushana na kujaribu kuangalia hesabu ya mabao.

Kuwaambia au kuwakumbusha Yanga kuwa sirias nafikiri ndio lilikuwa ni jambo muhimu zaidi. Kwa kuwa ushindi katika mechi mbili lilikuwa ni jambo linalowezekana kabisa.
Hata baada ya mechi ya kwanza, ushindi wa mabao 2-0, sote tuliona ilistahili zaidi kwa kuwa bila ubishi Asas si saizi ya Yanga na walipata nafasi ya kucheza na Yanga kwa kuwa tu ni mabingwa wa Djibouti.

Kama ungesema uwape nafasi ya kucheza na timu yoyote ya Ligi Kuu Bara, sijui kama wangepata nafasi ya kutoka. Hata kama wangejitahidi kufungwa 1-0 na 1-0 kwa kila mechi lakini wasingesonga mbele.

Kitu kizuri Yanga wameonyesha hawakuwa wakitaka mchezo katika mechi hiyo, jambo ambalo ni zuri zaidi kwa ajili ya mechi zinazofuata na hili ndilo linapaswa kuangaliwa.

Kama ni sehere ya kumfunga ASAS inaendelea, basi hii waachiwe mashabiki na wachezaji wajue mechi imeisha na sasa kama ni Caf Champions League inakwenda kuanza.

Ni kama historia inataka kufanana hivi lakini kuna baadhi ya sehemu chache sana inapishana. Angalia, msimu uliopita, Yanga ilianzia hatua ya awali kama hivi na mwisho ikaishia kufika fainali ya Kombe la Shirikisho ambalo lilibebwa na USM Alger ya Algeria.

Mechi ya kwanza, Yanga walipangwa na Zalan ya Sudan Kusini ambao ndio wanajitafuta kuutengeneza  mpira wao. Mechi mbili zote zikachezwa jijini Dar es Salaam na Yanga wakashinda kwa jumla ya mabao 9.

Mechi dhidi ya ASAS ambao pia Djibouti wanaendelea kujitafuta kuuamsha mpira wao wamefungwa jumla ya mabao 7.

Kulikuwa na tofauti ya ubora wa kiwango kati ya ASAS na Zalan na imejionyesha lakini bado ni timu zinazofanana. Msimu uliopita, Yanga baada ya kuingia hatua ya kwanza tu wakakutana na vigogo wa Sudan ambao ni Al Hilal.

Sare ya 1-1 jijini Dar na ushindi wa bao 1-0 kwao Kharthoum, ukawavusha Hilal na Yanga wakaporomoka hadi Kombe la Shirikisho ambako walianzisha safari mpya.

Safari hii, wanakwenda kukutana na vigogo wengine wa Sudan, El Merreikh ambao watakuwa na bahati mbaya ya kutowapata mashabiki kama itakuwa hivyo kutokana na machafuko nchini Sudan.

Mabadiliko sasa hakuna kwenda Kombe la Shirikisho la njia ambayo wanapita tena Yanga ni ileile na hii itawapa faida kwa kuwa watakuwa wamejifunza jambo kutokana na njia waliyopita msimu uliopita.

Ndio maana nimeweka msisitizo, kusiwe na sherehe kubwa kuwatoa ASAS wakati sote tumewaona. Tufurahie kwa kuamini Yanga wamelifanyia jambo hilo kazi kwa ufasaha na suala la sherehe kama wanataka kuendelea nalo mashabiki lakini wachezaji watambue Ligi ya Mabingwa Afrika, inakwenda kuanza sasa.

Lazima kujipanga, lakini kupadilisha mentality kuwa mpinzani anayefuata si aliyepita na kadhalika. Na inawezekana kwa kuwa timu inaweza kujipanga kulingana na uhalisia.

Previous articleAZAM FC YAIPIGA BAO YANGA KATIKA HILI
Next articleKOCHA SIMBA APEWA DAKIKA 180