ANAYECHEKA MWISHO HUYO HUCHEKA ZAIDI

    KIKOSI cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga kete yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu Bara ilikuwa ni Agosti 23 Uwanja wa Azam Complex.

    Kwenye mchezo huo ilishuhudia ubao ukisoma Yanga 5-0 KMC ukiwa ni mchezo uliokusanya mabao mengi ndani ya dakika 90 kwenye mechi za ufunguzi msimu wa 2023/24.

    Yanga iliingia katika mchezo huo ilitoka kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya ASAS katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ulipigwa Jumapili iliyopita.

    Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi huo ambao kikanuni ulikuwa ni ushindi wa ugenini na wanatarajiwa kucheza mchezo wa marudiano baada ya siku saba yaani Jumapili ya wiki hii.

    Ikiwa Yanga watavuka hatua hiyo, basi watakuwa tayari wamefuzu hatua ya kwanza ya mashindano hayo ambayo malengo makubwa kwao yamekuwa ni kufuzu hatua ya makundi ambayo hawajafanikiwa kufuzu kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

    Bila shaka matarajio ni makubwa kwa Yanga kwa kuwa msimu uliopita katika mashindano ya kimataifa walifanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo waliibuka washindi wa pili wa mashindano hayo.

    Pongezi kubwa kwa uongozi wa Yanga, benchi la ufundi, wachezaji pamoja na mashabiki wa klabu hiyo kwa mafanikio makubwa ambayo walifanikiwa kuyapata msimu uliopita.

    Ikumbukwe msimu uliopita Yanga waliondolewa mapema katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na ni wazi msimu huu hawatahitaji kurudia makosa, katika hili ni lazima Yanga wakumbuke ule msemo wa waswahili kuwa anayecheka mwisho ndiye anacheka zaidi.

    Yanga wasidhani ya kuwa wamemaliza kwa kuwa tu, wamepata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wao wa mkondo wa kwanza dhidi ya ASAS, lakini wajipange kucheza nao kwa tahadhari katika mchezo wa marudiano.

    Ni wazi wengi hawakutegemea Yanga kuondolewa mapema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, hususani kutokana na usajili bora ambao waliufanya mwanzoni mwa msimu.

    Lakini kilichotokea baada ya mapito hayo yote ni historia kwa timu hii, ambayo ni miongoni mwa timu mbili zenye mashabiki wengi zaidi Tanzania.

    Wanayanga walikubali kuwa yaliyotokea yametokea na kuamua kujikita katika kilichosalia mbele yao yaani Kombe la Shirikisho na kufanikiwa.

    Hili liwaendee Singida Fountain Gate FC ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKU ya Zanzibar, huku Azam wao wakipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Bahir Dar ya Ethiopia.

    Ikumbukwe wawakilishi wa kimataifa wanahitaji zaidi ya majina makubwa ya nchi ambazo waliweka kambi kama ilivyokuwa Tunisia na Uturuki.

    Binafsi nadhani mabenchi ya ufundi ya wawakilishi hawa wa kimataifa wanapaswa kuhakikisha wachezaji kutunza ‘focus’ yao na kutobweteka na mafanikio waliyoyapata bali wapambane zaidi katika michezo hii ya marudiano.

    Ni wazi kama watakubali kufanya kosa la kuamini kuwa tayari kazi imeisha kwa kuangalia matokeo ya mchezo wa mkondo wa kwanza basi watakumbushwa ule msemo wa “anayecheka mwisho, ndiye hucheka zaidi”.

    Kila la kheri wakimataifa.

    ReplyForwar

     

    Previous articleMUDA WA MIPANGO NI SASA LIGI INAHITAJI NGUVU
    Next articleGAMONDI AFUNGUA BUSTA LOTE, KIUNGO AOMBA KUVUNJA MKATABA SIMBA