NANI KUVUNJA REKODI YA MAYELE YANGA?

  USIKU wa deni haukawii kukucha, ndivyo unavyoweza
  kusema kwani hatimaye kivumbi cha mashindano ya
  kimataifa yaani Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la
  Shirikisho Afrika kimeanza kutimua vumbi rasmi Ijumaa na kinatarajiwa kuendelea wikiendi hii.

  Kwa upande wa Tanzania Bara msimu huu tunatarajiwa
  kushirikisha timu nne katika mashindano hayo, ambapo
  timu za Yanga na Simba zinatarajiwa kutuwakilisha katika
  mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC
  na Singida Fountain Gate zikituwakilisha kwenye Kombe
  la Shirikisho.

  Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba wao
  wana faida ya kuanzia hatua ya kwanza, hivyo ni watani
  zao wa jadi Yanga ambao wataanzia hatua hii ya awali
  ambapo karata yao ya kwanza itakuwa kuvaana na AS Ali
  Sabieh Djibouti Télécom (ASAS), ya Djibout ambapo
  mchezo wa mkondo wa kwanza utapigwa leo Jumapili
  kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

  Hapa tunakuletea dondoo muhimu za
  mchezo huu kama ifuatavyo,

  Ugenini kama nyumbani, nyumbani ni nyumbani tu

  Kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita dhidi ya Zalan, Yanga msimu huu pia wamepata mteremko wa michezo
  yao yote miwili ya hatua ya awali kupigwa kwenye ardhi
  ya Tanzania kutokana na maombi ya Zalan ambao
  wameomba kutumia Uwanja wa Azam Complex, kama
  Uwanja wao wa nyumbani.

  Kwa wapenzi wa ngumi hii inaweza kuwakumbusha ule
  usemi wa bondia maarufu, Karim Mandonga ambaye
  aliwahi kusema yeye akipigwa kama amepiga, na akipiga
  ndo amepiga. Hivyo kwa Yanga ugenini kama nyumbani,
  na nyumbani ni nyumbani tu.

  Nani kuvunja rekodi ya Mayele?

  Msimu uliopita kwenye kikosi cha Yanga bao la kwanza kwenye mashindano ya kimataifa lilifungwa na aliyekuwa
  straika wao mkongomani, Fiston Kalala Mayele akitumia asisti matata ya Denis Nkane dakika ya 45 ya mchezo ambao ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 huku Mayele akifunga Hat-trick.

  Kwa sasa Mayele hayuko ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kukamilisha uhamisho wa kujiunga na Pyramid FC ya
  Misri. Ukiachana na straika Mzambia, Kennedy Musonda

  Yanga imesajili straika mpya, Hafiz Konkon na swali kubwa ni je, nani atavunja rekodi ya Mayele? Ikumbukwe, Mayele pia msimu uliopita alimaliza akiwa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akiweka kambani mabao saba na kumzidi Ranga Chivaviro.

  Rekodi zinawabeba Yanga

  Licha ya kwamba wamekuwa na rekodi mbovu ya zaidi ya
  miaka 20 kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya
  Mabingwa Afrika lakini katika mizania Yanga
  wanaonekana kuwa kwenye faida kubwa ya rekodi nzuri
  za ushiriki wao kimataifa kulinganisha na wapinzani wao.

  Mafanikio makubwa ya Yanga katika mashindano ya
  kimataifa ni kuibuka washindi wa pili wa Kombe la
  Shirikisho Afrika, rekodi ambayo wamefanikiwa kuipata
  msimu uliopita ambapo waliukosa ubingwa wa
  mashindano hayo kutokana na faida ya kanuni ya bao la
  ugenini.

  Kwa upande wa ASAS ambao licha ya kwamba hakuna
  taarifa nyingi kuwahusu kwenye mtandao lakini ni inaonekana hawana rekodi yoyote ya kuweza kucheza hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa japo kwa nyakati kadhaa wamefanikiwa kutawala soka la ndani na
  kushinda ubingwa wa Ligi Kuu.

  Yanga wanasemaje?

  Kuelekea mchezo huo dhidi ya ASAS, Ofisa habari wa
  Yanga, Ali Kamwe: “Nadhani mchezo huu utakuwa
  mgumu zaidi kwetu kulinganisha na michezo ya Ngao ya
  Jamii kwa kuwa hatuna taarifa nyingi kuwahusu
  wapinzani wetu.

  “Tutahitaji kuwajibika zaidi kwenye mchezo huu na
  kusahau kuhusu Ngao ya Jamii  ili kutimiza malengo ya
  kufuzu hatua inayofuata.”

  Previous articleSIMBA 1-0 DODOMA JIJI, UWANJA WA UHURU WANAPATA TABU
  Next articleSIMBA YAKOMBA POINTI TATU MBELE YA WALIMA ZABABI